Hospitali ya Taifa Muhimbili ipo tayari kushiriki Msimu wa Tatu wa Kambi ya Matibabu Bure Mkoa wa Arusha, ambapo itatoa huduma za upasuaji wa macho bila malipo kwa wananchi.
Akikagua maandalizi ya mwisho ya kambi hiyo, Waziri wa Habari, utamaduni, sanaa na michezo na Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Paul Makonda, amewahimiza wananchi wa Arusha na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma mbalimbali zitakazotolewa na hospitali Muhimbili katika kambi hiyo
Mhe. Makonda amesema kambi hiyo ni fursa kwa wananchi kupata huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi bila malipo. Ameongeza kuwa ushiriki wa taasisi za afya, ikiwemo MNH, unaonyesha dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi.
Katika kambi hiyo, Muhimbili itatoa huduma za upasuaji wa mtoto wa jicho kwa watu wazima bila malipo kuanzia tarehe 13 hadi 19 Julai 2026 katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid. Wananchi wenye changamoto za macho zinazohitaji huduma hiyo wanakaribishwa kufika kwa ajili ya uchunguzi na matibabu, kwa lengo la kurejesha uwezo wa kuona na kuboresha ubora wa maisha yao.







0 Comments