NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA.
Matumizi ya mbolea hai yanayoenezwa na maafisa kilimo kupitia programu ya jenga kesho iliyo bora (BBT) yameibua matumaini mapya kwa wakulima wa zao la pamba katika kijiji cha Sayu, Kata ya Pandagichiza wilaya ya Shinyanga, huku yakichangia kuongeza la uzalishaji, kuboresha afya ya udongo na kuimarisha kipato cha wakulima
Mkulima wa mfano Philipo Lunebula Lili amesema matumizi ya mbolea hai pamoja na kufuata kanuni bora za kilimo vimemwezesha kuvuna kilo 2,174 za pamba kwa ekari moja msimu uliopita, tofauti na awali alipokuwa akilima kwa mazoea na kupata mavuno madogo.
Amesema mafanikio hayo yametokana na elimu inayotolewa na Serikali kupitia wataalamu wa kilimo na Bodi ya Pamba Tanzania, ambayo imewajengea uwezo wa kutumia teknolojia na mbinu bora za uzalishaji.
Philipo amesema mafanikio hayo yamempa hamasa ya kupanua eneo la kilimo na anaamini anaweza kuwa miongoni mwa wakulima bora nchini endapo ataendelea kuzingatia ushauri wa wataalamu.
Aidha amesema zaidi ya wakulima 30 wamepata elimu kutoka kwake kuhusu matumizi ya mbolea hai na kanuni bora za kilimo cha pamba, hatua inayochangia kuongeza tija katika kijiji hicho.
Naye mkulima Simba Cyprian amesema matumizi ya mbolea hai yameboresha ukuaji wa mimea na kuongeza matumaini ya kufikia mavuno ya kilo 3,000 kwa ekari katika msimu huu wa kilimo.
Hata hivyo amesema bado wakulima wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kupulizia dawa, hali inayowalazimu kutumia vifaa vya kawaida ambavyo hupunguza ufanisi.
Kwa upande wake, Tekera Mashauri amesema mbolea hai imewasaidia wakulima kukabiliana na athari za ukame kwa kuimarisha rutuba ya udongo na ukuaji wa mazao, huku kilimo cha pamba kikimwezesha kuinua uchumi wa familia yake na kumsomesha mtoto wake hadi kufikia chuo kikuu.
Andrea Maganga, pia ni mkulima wa kijiji cha Sayu amesema mbolea hai imechangia kupunguza mashambulizi ya baadhi ya wadudu waharibifu, kuimarisha ukuaji wa mimea na kuongeza idadi ya matunda ya pamba shambani.
Afisa wa BBT kutoka kijiji cha Sayu, Hery Mutabazi Renatus, amesema wakulima wanaozingatia maelekezo ya wataalamu kuhusu matumizi ya mbolea hai wameendelea kupata matokeo mazuri, huku juhudi zikiendelea kuwafikia wale ambao bado hawajafuata kanuni za kilimo bora.
Naye Afisa Kilimo wa kijiji cha Sayu, Bahati Maduhu, amesema mafunzo ya matumizi ya mbolea hai yamekwenda sambamba na elimu ya nafasi sahihi za upandaji, hatua iliyosaidia kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa kilo 400 hadi zaidi ya kilo 2,000 kwa ekari moja kwa baadhi ya wakulima.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Bodi ya Pamba Tanzania wilayani Shinyanga, Joachimu John Gobanya, amesema bodi imeendelea kusambaza pembejeo kwa wakati, kuimarisha huduma za ugani kupitia maafisa wa BBT na kuhamasisha matumizi ya mbolea hai ili kuongeza tija.
Amesema wilaya ya Shinyanga inatarajia kuvuna kilo milioni 3.5 za pamba katika msimu wa 2025/2026, ongezeko linalotokana na wakulima wengi kuzingatia kanuni bora za kilimo na kutumia teknolojia zinazoongeza uzalishaji.










0 Comments