Header Ads Widget

FILAMU ZA KISWAHILI ZA TANZANIA KUONYESHWA TV YA UFARANSA


Alain Kisena Mwakilishi wa TV5 Monde

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Filamu  za Kiswahili za Tanzania (Bongo Movies) pamoja na vipindi vya vichekesho (Comedy Show) vinavyoandaliwa na wasanii wa Tanzania zinatarajia kuanza kuonyeshwa kwenye tv na mitandao ya kijamii ya nchini Ufaransa ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani.


Hayo yameelezwa mjini Kigoma mwishoni mwa wiki na Mwakilishi wa kituo cha Tv cha TV5 Monde ya Ufaransa, Alain Kisena wakati wa mkutano na waandishi wa habari ambapo amesema  kuwa mpango huo unalenga kutoa nafasi kubwa zaidi kwa kazi za wasanii wa Tanzania kufikia watazamaji wengi duniani  kupitia jukwaa la televisheni hiyo.


Kisen alisema kuwa kupitia chaneli ya TV5Monde na mitandao yake ya kijamii inayofikia zaidi ya watu milioni 200 duniani, filamu za Kiswahili za Tanzania pamoja na vipindi vya vichekesho vitapata fursa ya kutazamwa na hadhira kubwa ya kimataifa ambapo  maudhui hayo ya lugha ya Kiswahili yatatafsiriwa kwa kutumia nukuu (subtitles) ya lugha za Kifaransa na Kiingereza.


Mwakilishi huyo wa TV5 Monde alisema kuwa wakati maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani yakitarajia kufanyika Julai saba katika Mji wa Paris nchini Ufaransa mpango huo ambao utakabidhiwa kwa uongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Julai sita mwaka huu ili mpango huo uwe sehemu ya ratiba ya maadhimisho hayo.


Inaelezwa kuwa mpango huo unatarajiwa kuongeza uelewa wa watazamaji kutoka mataifa mbalimbali na kukuza usambazaji wa kazi za wasanii wa Tanzania duniani, kufungua masoko mapya kwa tasnia ya filamu na burudani ya Tanzania.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI