Header Ads Widget

BIDHAA ZA NGOZI KUWAFUNGULIA FURSA VIJANA NCHINI .

 Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza imeendelea kuthibitisha ubora wake katika ubunifu na maendeleo ya teknolojia baada ya kushiriki kwa mafanikio katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) 2026, yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Maonesho haya yamewakutanisha maelfu ya washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania, yakitoa jukwaa la kuonesha bidhaa, huduma, ubunifu na teknolojia zinazochochea maendeleo ya viwanda, biashara na uchumi wa taifa.




















Katika banda la DIT, wageni wengi wamejitokeza kushuhudia bunifu mbalimbali za kiteknolojia zilizobuniwa na wanafunzi na wataalamu wa taasisi hiyo. Miongoni mwa bunifu zilizovutia zaidi ni bidhaa za ngozi zinazotengenezwa na DIT Kampasi ya Mwanza, zikiwemo viatu, pochi, wallet, mikanda, mipira pamoja na bidhaa nyingine zenye ubora wa hali ya juu.


Akizungumza katika maonesho hayo, Mhadhiri msaidizi wa DIT Kampasi ya Mwanza, Mha. Sharif Mwangi, amesema mwitikio mkubwa wa wageni unaonesha kuwa bidhaa zinazozalishwa na wanafunzi wa DIT zina ubora unaokidhi mahitaji ya soko na zina uwezo wa kushindana kimataifa.


Amesema DIT inaendelea kutoa elimu ya vitendo inayowajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri na kuanzisha viwanda vidogo kupitia uchakataji wa ngozi na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zenye thamani.


Aidha, mha. Mwangi amebainisha kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mradi wa EASTRIP, ambapo kampasi ya Mwanza ilipokea takribani shilingi bilioni 37 zilizotumika kuboresha miundombinu ya kufundishia, kununua mashine za kisasa, kuimarisha maabara za kiasasa,Hosteli pamoja na kuwawezesha wahadhiri kuongeza ujuzi katika maeneo mbalimbali ya teknolojia katika vyuo vya ndani na nje ya Tanzania

"Ninawakaribisha sana wazazi na wanafunzi kujiunga na DIT ili kupata ujuzi wa kuchakata ngozi na kutengeneza bidhaa mbalimbali zenye ubora.


Ujuzi huu unawawezesha wahitimu kujiajiri, kuanzisha biashara zao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi," amesema mha. Mwangi.


Kwa upande mwingine, moja ya bunifu zilizopata pongezi nyingi kutoka kwa wageni ni kiatu cha sandal chenye mikanda inayoweza kubadilishwa, kilichobuniwa na mwanafunzi wa DIT, Arnold Kimaro.

Arnold amesema ubunifu huo unamwezesha mtumiaji kubadili mikanda ya kiatu kulingana na mahitaji au mavazi yake, hivyo kuonekana kana kwamba anavaa viatu tofauti bila kulazimika kubeba jozi nyingi, hususan wakati wa safari au akiwa ofisini.

Ameongeza kuwa kiatu hicho kinauzwa kwa bei nafuu ya Shilingi 35,000 na tayari kimevutia wateja wengi wanaotembelea banda la DIT kutokana na ubunifu wake, ubora na matumizi yake ya kisasa.

Ushiriki wa DIT katika Maonesho ya SABASABA 2026 umeendelea kuonesha nafasi ya taasisi hiyo katika kukuza ubunifu, teknolojia na ujuzi wa vitendo, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda kupitia wataalamu wenye maarifa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye thamani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI