Na Samwel Mwanga, Maswa.
WANANCHI wa vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wameandika historia mpya baada ya kuchangishana fedha na kufanikiwa kutengeneza jumla ya madawati 3,500 kwa ajili ya shule za msingi zilizopo wilayani humo, hatua inayolenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutatua changamoto ya wanafunzi kukaa chini darasani.
Akizungumzia mafanikio hayo katika Kijiji cha Chugambuli, Kata ya Nguliguli, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vincent Naano, amesema kampeni hiyo ilianzishwa baada ya kubaini uwepo wa upungufu wa samani za shule katika baadhi ya maeneo na kuamua kuwahamasisha wananchi kushiriki kutatua changamoto hiyo.
Amesema mwitikio mkubwa wa wananchi umewezesha kutengenezwa kwa madawati hayo kwa muda mfupi, jambo ambalo litapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanafunzi waliokuwa wakisomea chini.
“Lengo letu lilikuwa kuhakikisha kila mtoto anapata mazingira bora ya kujifunzia. Wananchi wameonyesha uzalendo mkubwa na moyo wa kujitolea katika kuunga mkono juhudi za Serikali,” amesema Dkt Naano.
![]() |
Amesema Wilaya ya Maswa ina upungufu wa madawati 11,243 katika shule za msingi, hivyo wananchi wamejipanga kutengeneza madawati 8,000 kwa nguvu zao, huku Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ikitarajia kutengeneza madawati 5,000 ili kuondoa kabisa changamoto ya wanafunzi kukaa chini wakiwa madarasani.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha (kushoto) akiwa na Mkuu wa wilaya ya Maswa Dk Vicent Naano (kulia) wakiwa wamekaa kwenye madawati yaliyotengenezwa na wananchi katika kijiji cha Chugambuli wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga.Baadhi ya wananchi walioshiriki katika mpango huo wamesema waliguswa na hali ya wanafunzi kukosa samani za kutosha shuleni na kuamua kuchukua hatua kwa pamoja.
Mkazi wa Kijiji cha Chugambuli, Rehema Jilala, amesema wananchi waliona umuhimu wa kusaidia watoto wao kupata mazingira bora ya kujifunzia badala ya kusubiri msaada kutoka nje pekee.
“Tumefanya hivi kwa moyo wa kujitolea kwa sababu elimu ni msingi wa maendeleo. Tuliona watoto wetu wanahitaji madawati na tukaamua kuunganisha nguvu kuhakikisha wanasoma katika mazingira mazuri,” amesema.
Naye Joseph Ngulimi, mkazi wa kijiji hicho, amesema ushirikiano uliooneshwa na wananchi umeonyesha kuwa jamii ina uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili watoto wao inapopata uhamasishaji sahihi.
“Wananchi wamechangia fedha, vifaa na nguvu kazi. Huu ni mfano mzuri wa namna jamii inavyoweza kushiriki maendeleo ya sekta ya elimu,” amesema.
Akikabidhiwa rasmi madawati hayo na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amewapongeza wananchi wa Maswa kwa hatua hiyo na kueleza kuwa imeleta faraja kubwa kwa Serikali kutokana na mchango wao katika kuboresha sekta ya elimu.
Macha amesisitiza umuhimu wa kuyatunza madawati hayo ili yaweze kudumu na kuwanufaisha wanafunzi kwa muda mrefu, huku akieleza kuwa ushirikiano ulioonyeshwa na wananchi wa Maswa unapaswa kuigwa na wilaya nyingine za mkoa huo.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chugambuli wilaya Maswa waliomaliza kutengeneza madawati kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi Chugambuli.Picha na Samwel Mwanga.“Kitedo hiki kinaonyesha kuwa maendeleo yanawezekana pale wananchi wanapoungana na kushiriki kikamilifu katika kutatua changamoto zinazowakabili. Nawapongeza sana wananchi wa Maswa kwa mfano huu mzuri,” amesema.
Amesema hatua hiyo ni ushahidi wa mshikamano na uwajibikaji wa wananchi katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha mazingira ya elimu na kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujifunza katika mazingira bora na salama.
Mwisho.









0 Comments