Header Ads Widget

TFS KUIMARISHA UHIFADHI WA MICHORO YA KONDOA KWA KUZIENDEA FURSA ZA UNESCO

 *


Na Mwandishi Wetu, Kondoa


KONDOA. Tanzania imeelezwa kuwa na fursa kubwa ya kuimarisha uhifadhi na kuendeleza utalii katika Kituo cha Michoro ya Miambani Kondoa Irangi kupitia ushirikiano na UNESCO na wadau wa kimataifa, huku maandalizi ya miradi maalumu yakitajwa kuwa njia muhimu ya kupata fedha, utaalamu na vifaa vya kisasa vya uhifadhi.

Kauli hiyo imetolewa, Agosti 15, 2026, na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Said Athman Ayubu, alipotembelea kituo hicho kilichopo wilayani Kondoa kwa lengo la kujionea hali ya uhifadhi na shughuli za utalii katika eneo hilo lililotambuliwa kuwa Urithi wa Dunia.

Balozi Ayubu amepongeza Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa hatua zilizochukuliwa kuimarisha uhifadhi wa michoro hiyo pamoja na kuboresha miundombinu na mazingira ya kuhudumia watalii, akisema hali ya michoro hiyo inaonesha juhudi zinazofanyika kulinda urithi huo muhimu.

Hata hivyo, alisema mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuwa changamoto inayohitaji utaalamu na teknolojia zaidi, hivyo TFS inapaswa kutumia fursa zilizopo kwa kuandaa miradi maalumu ya uhifadhi itakayowezesha Tanzania kupata ufadhili, utaalamu, vifaa kutoka UNESCO na wadau wengine wa kimataifa.

“Tujitahidi kuandika mradi maalumu ili tuweze kupata ufadhili, utaalamu na vifaa pale inapohitajika,” alisema Balozi Ayubu, akisisitiza umuhimu wa kutumia fursa za ushirikiano wa kimataifa katika kuendeleza eneo hilo.

Balozi huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kundi la Afrika (African Group) katika utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Urithi wa Dunia, alisema nafasi hiyo inaweza kutumika kuongeza ushirikiano na kuishawishi Afrika kuiunga mkono Tanzania katika juhudi za kuimarisha uhifadhi wa maeneo yake ya Urithi wa Dunia.

Kituo hicho kinaendelea kuwa miongoni mwa vivutio muhimu vya utalii wa urithi nchini, ambapo watalii wapatao 7,000 wa ndani na nje ya nchi walitembelea eneo hilo mwaka jana, jambo linaloonesha fursa yake katika kukuza utalii na uchumi wa eneo la Kondoa.

Ziara hiyo imekuja wakati Tanzania ikiendelea kuimarisha uhifadhi wa maeneo yake ya Urithi wa Dunia, huku Kondoa ikiwa miongoni mwa maeneo saba nchini yaliyotambuliwa na UNESCO, pamoja na Ngorongoro, Kilimanjaro, Selous, Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, Serengeti na Mji Mkongwe wa Zanzibar.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI