Hospitali ya Taifa Muhimbili imefanya upasuaji ndani ya Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba kwa kutumia gari la kisasa la upasuaji kwa kumfanyia upasuaji mgonjwa aliyesumbuliwa na uvimbe kwenye kucha na kusababisha maumivu makali.
Hatua hiyo inaonesha uwezo wa hospitali wa kusogeza huduma za kibingwa na kibingwa bobezi karibu na wananchi kupitia teknolojia ya kisasa.
Gari hilo la kisasa la upasuaji lina vifaa vinavyokidhi viwango vya utoaji wa huduma salama za upasuaji, hivyo kuwezesha huduma kutolewa nje ya mazingira ya kawaida ya hospitali bila kuathiri ubora wa matibabu.
Hatua hiyo inaakisi dhamira ya Hospitali hiyo ya kuendelea kuboresha huduma za afya kwa kutumia ubunifu na teknolojia za kisasa, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi nchini.
MNH inawakaribisha wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba ili kupata huduma mbalimbali za uchunguzi, ushauri wa kitaalamu na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa na bingwa bobezi, pamoja na kujionea teknolojia mbalimbali zinazoboresha utoaji wa huduma za afya nchini.









0 Comments