Na Mwandishi Wetu.
MKURANGA, PWANI, Juni 30, 2026 – Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Mashariki, inayohudumia mikoa ya Pwani, Morogoro na Tanga, limeteketeza tani 4.5 za bidhaa hafifu na zilizopigwa marufuku zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 25 katika zoezi lililofanyika eneo la Mbezi Gongoni, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Bidhaa zilizoteketezwa ni taulo na nguo za ndani za mitumba ( ambazo kisheria haziruhusiwi kuingizwa nchini ), vipodozi vilivyopigwa marufuku, bidhaa za chakula zilizokwisha muda wa matumizi pamoja na rangi ambazo hazikukidhi matakwa ya viwango vya ubora na zilizokwisha muda wa matumizi ( expired ).
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi hilo, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, Mhandisi Saireal Kimario, alisema bidhaa hizo zilipatikana kupitia ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na shirika hilo katika masoko, maduka na maeneo mbalimbali ya biashara ndani ya mikoa inayohudumiwa na kanda hiyo.
Alisema bidhaa hizo ziliondolewa sokoni na kuteketezwa ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kwa watumiaji pamoja na kulinda mazingira ya biashara kwa kuhakikisha bidhaa zinazopatikana sokoni zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
Mhandisi Kimario amewasihi wananchi kuzingatia ununuzi wa bidhaa zenye viwango kwa kuhakikisha wanasoma taarifa muhimu zilizopo kwenye vifungashio, ikiwemo tarehe ya mwisho wa matumizi, pamoja na kutambua alama ya ubora ya TBS kabla ya kufanya matumizi.
Alisema ushiriki wa wananchi katika kuchagua bidhaa salama ni hatua muhimu ya kuvunja mnyororo wa bidhaa zisizofaa kuingia na kusambazwa nchini.
"Tunawaomba wananchi wawe makini wanaponunua bidhaa mbalimbali. Wanunuzi wanapaswa kuhakikisha bidhaa wanazotumia zinakidhi viwango na kutoa taarifa kwa TBS wanapobaini bidhaa zenye mashaka. Ushirikiano huo utatusaidia kuvunja mnyororo wa bidhaa zisizofaa nchini na kulinda afya ya jamii," alisema Mhandisi Kimario.
Aidha, amewataka wafanyabiashara kuzingatia sheria na viwango vinavyosimamiwa na TBS kwa kuacha kuuza bidhaa zisizokidhi matakwa ya ubora, vipodozi vilivyopigwa marufuku pamoja na bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi, akisisitiza kuwa shirika hilo halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria kwa makusudi.
Alieleza kuwa lengo la TBS si kuwaadhibu wafanyabiashara, bali kuhakikisha bidhaa zote zinazowafikia wananchi ni salama, zenye ubora unaokubalika na zinazokidhi viwango vya kitaifa, hivyo kulinda afya ya watumiaji, mazingira ya biashara na uchumi wa Taifa.
Shirika hilo limesisitiza kuwa litaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vingine vya dola ili kuhakikisha bidhaa zisizokidhi viwango hazipati nafasi ya kuingia sokoni.




























0 Comments