Header Ads Widget

SEKRETARIETI YA MAADILI YATAKA WADAU WASHIRIKIANE KUPAMBANA NA RUSHWA


Na Lilian Kasenene, Morogoro

Matukio DaimaApp 

SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewataka wadau kushirikiana katika kutoa elimu ya maadili kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi, ikiwemo rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.


Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi, amesema Sekretarieti inahitaji kushirikiana na wataalamu wa utoaji elimu kwa umma ili kufanikisha malengo ya kuimarisha maadili ya uongozi na utumishi wa umma.


"Kidole kimoja hakivunji chawa. Ndiyo maana tunahitaji kubadilishana mawazo na wataalamu wa utoaji elimu kwa umma kuhusu njia na mbinu bora za kutoa elimu hiyo kwa wananchi," alisema Kamishna Mwangesi.



Hotuba ya Kamishna Mwangesi ilisomwa kwa niaba yake na Katibu wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Omar Juma, wakati wa kikao cha wadau wa utoaji elimu kwa umma.


Katika hotuba hiyo, Kamishna Mwangesi alisema miongoni mwa changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ni matumizi mabaya ya madaraka kwa maslahi binafsi, mgongano wa maslahi, rushwa, vitendo vya upendeleo, pamoja na ukosefu wa uwazi na uwajibikaji katika kufanya maamuzi.

"Changamoto tunazotakiwa kukabiliana nazo kupitia elimu kwa wananchi na watumishi wa umma ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka kwa maslahi binafsi, mgongano wa maslahi, rushwa, vitendo vya upendeleo, pamoja na kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji katika maamuzi," alisema.


Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni kutotoa taarifa sahihi kwa umma pamoja na ukiukwaji wa misingi ya uongozi bora na maadili ya kazi.


Kwa upande wake, Katibu wa Idara ya Ukuzaji Maadili katika Ofisi ya Rais – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Omar Juma, alisema wadau wa utoaji elimu kwa umma wanapaswa kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi ili kujenga utamaduni wa ushirikiano na kuimarisha maadili.


Alisema pamoja na kutumia wataalamu wa utoaji elimu kwa umma, Sekretarieti pia hutumia majukwaa mbalimbali kufikisha elimu hiyo, ikiwemo mikutano, maonesho, machapisho, vyombo vya habari, semina na makongamano.


Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI