NA MATUKIO DAIMA MEDIA,MUFINDI
Licha ya kukumbana na changamoto nyingi za maisha ikiwemo kulea watoto wawili peke yake, kufanya kazi za ndani kwa miaka kadhaa na kukabiliwa na MERITA MHENI
umaskini wa familia, Merita Mheni wa kijiji cha Uhafilo, kata ya Mapanda wilayani Mufindi, ameendelea kupambana huku akiamini kuwa maisha bora yanawezekana kupitia juhudi na maarifa.
Merita anasema maisha yake yalianza kukumbwa na changamoto mapema baada ya kupata mtoto wa kwanza akiwa bado mdogo.
Baadaye baba wa mtoto huyo alimchukua na kumpeleka kwa bibi yake.
Alipopata mtoto wa pili na mwanaume mwingine, naye alimtelekeza na kumuachia jukumu la kulea mtoto huyo.
“Nina watoto wawili wa baba tofauti,Mtoto wa kwanza baba yake alimchukua na kumpeleka kwa bibi yake,Baadaye nikapata mtoto wa pili lakini baba yake naye alinitelekeza,Hivyo nimeendelea kuwalea watoto wangu mwenyewe,” anasema Merita.
Anasema pamoja na mtoto wa kwanza kuishi kwa bibi yake, bado amekuwa akihusika katika malezi yake kutokana na mazingira magumu ya familia hiyo.
Mbali na changamoto za malezi, Merita pia alikumbwa na matatizo ya kifamilia baada ya baba yake, ambaye alikuwa na ulemavu wa kutokuona, kufariki dunia mwaka jana,tangu wakati huo ameendelea kuishi na mama yake huku akijitahidi kuchangia mahitaji ya familia.
Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, Merita alielekea jijini Dar es Salaam kutafuta ajira za ndani,hata hivyo, anasema kazi hizo hazikumpatia maendeleo aliyokuwa akiyatarajia.
“Nilifanya kazi za ndani kwa takribani miaka miwili,Mara nyingi waajiri walikuwa wanaahidi kulipa baada ya miezi kadhaa, lakini wakati mwingine tulitofautiana na nikaondoka bila kupata malipo,Mshahara pia ulikuwa mdogo na haukuweza kukidhi mahitaji yangu na ya familia,” anasema.
Anabainisha kuwa baadhi ya mazingira ya kazi yalikuwa magumu kiasi cha kumkatisha tamaa na kumfanya aamue kurejea kijijini kuanza maisha mapya.
Akiwa kijijini, Merita alijikita katika shughuli za kilimo kwa ajili ya kujikimu,huku changamoto ya ardhi isiyo na rutuba ya kutosha pamoja na uhaba wa mashamba ilifanya uzalishaji kuwa mdogo na kutotosheleza mahitaji ya familia kwa mwaka mzima.
“Mara nyingi tulikuwa tunalima lakini mavuno hayakutosha,mahindi yalikuwa yanaisha mapema kabla ya msimu mwingine wa kilimo kufika,” anasema.
Matumaini mapya kwa Merita yalianza kujitokeza baada ya kufikiwa na mradi wa Youth Agency Mufindi (YAM), unaolenga kuwawezesha vijana na mabinti kupitia mafunzo mbalimbali ya maendeleo na ujasiriamali.
Kupitia mafunzo hayo, Merita anasema amepata mwamko mpya wa maisha na sasa ana ndoto ya kuwa fundi mshonaji ili aweze kujitegemea na kuboresha maisha ya familia yake.
“Ndoto yangu ni kuwa mshonaji,ninaamini elimu ninayoipata itanisaidia kujenga maisha bora na kuwa na kipato cha uhakika,” anasema.
Aidha, ametoa wito kwa mabinti wengine wanaokabiliwa na changamoto za maisha kutokata tamaa wala kukimbilia ajira za ndani mijini bila maandalizi mazuri.
“Nawashauri mabinti wenzangu waendelee kupambana na kutumia fursa zilizopo katika jamii zao.
Elimu na maarifa tunayopata yanaweza kutusaidia kubadilisha maisha yetu,” anasema.
Kwa sasa Merita anaendelea kushiriki mafunzo yanayotolewa kupitia mradi huo huku akiamini kuwa hatua hiyo itakuwa mwanzo wa safari mpya ya mafanikio kwake na familia yake.
Safari ya Merita ni mfano wa jinsi uvumilivu, juhudi na fursa za maendeleo zinavyoweza kumwezesha mtu kubadilisha maisha yake licha ya changamoto nyingi alizopitia.
Baada ya kurejea kijijini, Merita alijikita katika shughuli za kilimo kwa ajili ya kujikimu na kulea watoto wake.
Ingawa kilimo hicho hakikuwa cha biashara, kilimsaidia kupata chakula na kuendesha maisha ya kila siku.
Mabadiliko makubwa yalianza pale alipofikiwa na mradi wa Youth Agency Mufindi (YAM), ambao umekuwa ukitoa mafunzo na kuwawezesha vijana na mabinti katika jamii.
Kupitia mafunzo hayo, Merita alianza kuona matumaini mapya na kuota ndoto kubwa zaidi.
“Ndoto yangu ni kuwa fundi mshonaji,Naamini kupitia elimu ninayoipata sasa nitaweza kujenga maisha bora na kujitegemea,” anasema.
Merita anatoa shukrani kwa mradi wa YAM kwa kumpa fursa ya kujifunza na kujitambua,Pia anatoa wito kwa mabinti wengine kutokata tamaa wala kukimbilia kazi za ndani mijini bila mipango, kwani wanaweza kutumia fursa zilizopo vijijini kujiletea maendeleo.
“Nawashauri mabinti wenzangu wasikate tamaa. Wapambane na changamoto za maisha na watumie fursa zinazopatikana katika jamii zao.
Elimu tunayoipata kupitia mradi huu inaweza kutusaidia kubadilisha maisha yetu,” anasema.
Leo hii, Merita anaamini kuwa changamoto alizopitia zimemjengea nguvu na uzoefu. Anaendelea kupambana ili kutimiza ndoto yake ya kuwa mshonaji na kuboresha maisha ya watoto wake pamoja na familia yake.
Hakika, safari ya Merita ni ushahidi kuwa changamoto za maisha zinaweza kuwa daraja la kuelekea mafanikio pale mtu anapoamua kutokata tamaa na kuendelea kupambana.
Mradi wa YAM unatekelezwa na taasisi ya Foxes Community and Wildlife Conservation kupitia mradi mradi wa Youth Agency in Mufindi (YAM) na Halmashauri ya Mufindi chini ya ufadhili Deaconess Foundation, FCWC na MFA.








0 Comments