NA MATUKIO DAIMA MEDIA , MUFINDI
VIJANA 120 wanaoishi katika mazingira magumu wanaoishi vijiji vya pembezoni kata ya Mpanga Tazara na Mapanda wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wamedai moja ya changamoto wanazokumbana nazo na kushindwa kunufaika na fursa ya mikopo ya Halmashauri ni pamoja na kusosa namba ama vitambulisho vya NIDA.
Hayo yameibuka jana kijiji cha Igoda wakati wa uwasilishaji wa kazi za vikundi wakati wa mafunzo yanayoendelea ya Saikolojia na ujasiriamali yanayotolewa Foxes Community and Wildlife Conservation kupitia mradi mradi wa Youth Agency in Mufindi (YAM) na Halmashauri ya Mufindi chini ya ufadhili Deaconess Foundation, FCWC na MFA.
Wakiwasilisha changamoto zao mmoja wa vijana hao Adelika Kahise kutoka kijiji cha Mapanda alisema kuwa ukosefu wa kitambulisho cha Taifa (NIDA)huwafanya kukosa mikopo kutoka halmashauri na hivyo kukosa mitaji na kujiinua kiuchumi.
“Wazazi wangu walifariki nikiwa kidato cha kwanza hivyo sikuweza kuendelea na masomo na sikuwa na mahali pa kuishi,wengine walitelekezwa wakiwa wadogo,ndugu kukataa mabinti waliobeba mimba na kukataliwa na wahusika wa mimba hizo”alisema Adelika
Kwa upande wake alisema kuwa changamoto wanayokutana nayo ipo katika shughuli za kilimo ambapo kukosekana kwa pembejeo kwa wakati inafanya wanashindwa kulima kisasa na kupata mazao mengi.
“Vijana wengi vijijini tunalima bila kufuata utaratibu wa kilimo cha kisasa kutokana na kukosa pembejeo,tunalima kienyeji hatuweki mbolea wala kupiga dawa ikifika wakati wa mavuno unajikuta unavuna debe mbili ambayo hayatoshi kulisha familia”
Alieleza kuwa changamoto nyingine anayokutana nayo ni ukosefu wa kitambulisho cha NIDA kwa vijana kunachangia vijana kukosa fursa za mikopo na kushirikishwa katika mambo mengi kutokana na ukosefu wa NIDA.
Akizungumza Mtaalamu Mshauri katika mradi wa YAM Dkt Heriel Mfangavo amesema lengo la Mradi huo ni kuwawezesha vijana kuweza kutawala maisha yao kiuchumi,kifikra na kijamii na hasa inalenga kuwawezesha vijana kuweza kushughulikia changamoto zao.
Alisema kwa awamu hii wameibua vijana kutoka maeneo ya vijijini Mapanda na Mpanga Tazara ambapo tumegundua vijana hao wanapitia changamoto ya ukosefu wa fursa za kiuchumi na wengi wao wanatoka katika familia ambazo zimewatenga.
“Wengi wanakuwa wamepoteza wazazi wao wakafukuzwa sehemu walikuwa wanaishi na wengine kunyang’anywa ardhi na baadhi walishindwa kuendelea na shule kwa sababu wazazi walifariki ndugu wakashindwa kuwaendeleza,wapo waliomaliza na wapo mtaani wanafanya shughuli za kilimo ambacho kinategemea msimu”alisema
Alisema kuwa kutokana na changamoto hizo wengi hao huwapelekea kuwa na msongo wa mawazo na kujiingiza katika matumizi ya vilevi na tabia hatarishi.
“kwa awamu hii ya kwanza tunawasaidia kuwajengea uwezo wa kisaikolojia na kijamii katika kujiamini na kushughulikia changamoto ambazo wamezipitia awali, ambazo ndio zinamuunda kijana ambaye tuponaye hapa na endapo zisiposhughulikiwa zitaharibu utu uzima wake”alisema
Baada ya awamu ya kwanza ya mafunzo wataendelea na awamu ya pili ambayo yatajifunza ujasiliamali pamoja fursa zilizopo katika mazingira yao, watapata mafunzo ya kilimo na kuwezeshwa kubaini fursa za kupata mitaji.
“Wamelalamika kuhusu vitambulisho vya nida kwamba ni changamoto ambayo inawafanya wakose fursa za mikopo, hili tutalishughulikia kwa sababu mradi hii unafanya kazi na Wilaya ya Mufindi na uko bega kwa bega katika kuwaibua vijana na kuwawezesha,hivyo watapata nida na watapata fursa ya mikopo ya halmashauri”alisema
Matukio Daima Media imezungumza na mkuu wa wilaya ya Mufindi Dkt Linda Selekwa kuhusiana na chagamoto ya viyambulisho vya NIDA kwa vijana hao wilayani humu alisema anawasiliana na ofisi ya NIDA ili kuangalia uwezekano wa kusogeza huduma kwa vijana waishio pembezoni mwa mji ili wapewe huduma hiyo na kuweza kunufaika na fursa za mikopo .
MWISHO.






0 Comments