Header Ads Widget

CHUO CHA MAENDELEO YA JAMII RUNGEMBA NGUZO YA UJUZI, AJIRA NA MABADILIKO YA KIJAMII

 


Na Francis Godwin Matukio Daima Media Mufindi

CHUO cha Maendeleo ya jamii Rungemba wilaya ya Mufindi ni mkoani Iringa ni moja kati ya vyuo vya maendeleo ya jamii bora nchini vyenye dhamira ya dhati kukuza ujuzi wa kuongeza ajira kwa vijana.


Chuo hiki kimeendelea kuwa kimbilio la uhakika kwa watu wengi hasa vijana na mabinti kupata elimu ya ufundi.



Kama njia atika  ya  kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.

Aliyekuwa katibu mkuu wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia wanawake makundi maalum Dkt John Jingu amesisitiza umuhimu wa elimu ya vitendo na ujuzi katika kujenga kizazi chenye uwezo wa kujitegemea. 


Kauli hiyo aliitoa wakati wa ziara yake katika Chuo hicho hivi karibuni wakati  akizungumza na wahitimu wa fani ya ushonaji.


Dkt Jingu alisema kuwa mazingira ya sasa yanahitaji vijana kubadilika kimtazamo na kuacha kutegemea ajira za serikali pekee. Alifafanua kuwa ongezeko la vyuo pamoja na taasisi zinazotoa mafunzo, ikiwemo njia za mtandaoni, limeongeza ushindani mkubwa katika soko la ajira, hivyo kufanya kuwa vigumu kwa kila mhitimu kupata ajira rasmi serikalini.

“Ni muhimu kwa vijana kutumia fursa zilizopo kujiajiri na hata kuajiri wengine. Elimu ya ufundi kama ushonaji ni nyenzo muhimu ya kujikwamua kiuchumi,” alisema Dkt Jingu.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, alibainisha kuwa vyuo vya maendeleo ya jamii, ikiwemo Rungemba, vimeanza kutoa kozi fupi kwa wanajamii ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii. Aidha, aliupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuendeleza ujuzi na ubunifu kwa wanafunzi.

Aliongeza kuwa maelekezo ya Dkt Samia Suluhu Hassan yanasisitiza kuwa taasisi zote za mafunzo zinapaswa kuwa na mchango wa moja kwa moja kwa jamii. “Vyuo vinapaswa kuonyesha thamani yake kwa kushirikiana na jamii na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowazunguka,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Kidubya Kulamiwa, aliwasilisha taarifa inayoonyesha hali halisi ya jamii inayozunguka chuo hicho. Alisema kuwa asilimia 42 ya kaya zinakabiliwa na uhaba wa chakula, huku asilimia 15 ya watoto wenye umri wa kwenda shule hawapati elimu. Aidha, asilimia 76.5 ya wazee hawapati msaada wa kijamii na kiuchumi.

Kulamiwa alibainisha pia kuwa changamoto za kifamilia, ikiwemo wazazi kutowajibika, zimekuwa zikichangia matatizo ya kijamii, huku asilimia 79 wakikiri kuwepo kwa changamoto katika mawasiliano kati ya wazazi na watoto.

Katika kukabiliana na hali hiyo, chuo hicho kinaendesha programu mbalimbali za uendelezaji ujuzi, ikiwemo programu ya uanagenzi. Kwa mwaka 2026, chuo kimefanikiwa kushirikiana na wadau 32 wanaoweza kupokea wanafunzi kwa mafunzo ya vitendo, ambapo wanafunzi 16 tayari wameunganishwa na wadau hao huku lengo likiwa kufikia wanafunzi 100.

Hata hivyo, Kulamiwa alitaja changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, zikiwemo uchakavu wa miundombinu, uhaba wa mabweni na madarasa, pamoja na kusimama kwa ujenzi wa maabara na chumba cha kompyuta ulioanza mwaka 2023 kutokana na ukosefu wa rasilimali.

Wanafunzi wa chuo hicho wameeleza kuridhishwa na mafunzo wanayopata, wakisema yanawasaidia kujitegemea badala ya kusubiri ajira. Juliana Samson kutoka Mwanza alisema kuwa amepata ujuzi wa ushonaji ambao utamwezesha kujiajiri mara baada ya kuhitimu.

Kwa upande mwingine, Anna Nyangasi alieleza jinsi chuo hicho kilivyomsaidia kupata elimu pamoja na mtaji wa kuanzia biashara ya ushonaji. “Tumepata elimu na vifaa vinavyotuwezesha kujitegemea. Tunamshukuru Rais kwa fursa hii,” alisema.

Mbali na masuala ya ajira, chuo hicho pia kimejikita katika kupambana na changamoto za kijamii kama ukatili wa kijinsia na lishe duni. Dkt Jingu alieleza kuwa chuo cha Rungemba kimekuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii kwa kushirikiana na serikali za mitaa na wanajamii.

Kupitia dawati la jinsia lililoanzishwa chuoni hapo, wanajamii pamoja na wanafunzi wanapata msaada na elimu kuhusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia. Jitihada hizo pia zinahusisha kubadili mila na desturi potofu zinazochangia vitendo hivyo.

Katika eneo la lishe, chuo kinafanya kazi kwa karibu na jamii kuhamasisha matumizi ya vyakula vinavyopatikana kwa urahisi ili kuboresha afya, hasa kwa watoto. Elimu hiyo inalenga kupunguza udumavu na kuboresha ukuaji wa watoto kiakili na kimwili.


Magdarena John Magala alieleza fahari yake ya kusoma katika chuo hicho na kuahidi kutumia maarifa aliyopata kuitumikia jamii. Vivyo hivyo, Hilda Ngwale alisema uwepo wa chuo hicho umeleta fursa kubwa kwa mabinti kujifunza na kujitegemea kiuchumi.

Penina Kalinga alisisitiza umuhimu wa kupambana na ukatili wa kijinsia ili jamii iweze kunufaika kikamilifu na fursa za maendeleo zinazotolewa na chuo hicho.

Kwa upande wa serikali za mitaa, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mafinga Mji alieleza kuwa chuo hicho kina mchango mkubwa katika kupunguza ukatili wa kijinsia na kutoa elimu ya lishe kwa jamii. Pia alisisitiza umuhimu wa kuunga mkono juhudi za Dorothy Gwajima katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatoweka nchini.

Kwa ujumla, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba kimeendelea kuwa mfano bora wa taasisi inayochangia maendeleo ya jamii kwa vitendo. 

Mkuu wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba wilayani Mufindi Kidubya Kulamiwa (kushoto) akimkabidhi zawadi ya mkoba wa ngozi uliotengenezwa na wanafunzi chuo hicho ,katibu mkuu  wizara ya maendeleo ya jamii,wanawake na makundi maalum Dkt John Jingu jana baada ya kufanya ziara chuoni hapo picha na Matukio Daima Media


Kupitia elimu ya ujuzi, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, pamoja na juhudi za kuboresha lishe, chuo hicho kinajenga msingi imara wa maendeleo endelevu katika wilaya ya Mufindi na maeneo jirani.


Chuo cha Rungemba ni  dhahiri kuwa uwekezaji katika elimu ya vitendo na ushirikiano kati ya taasisi na jamii ni nguzo muhimu katika kujenga taifa lenye vijana wanaojitegemea na jamii yenye ustawi.


Makala haya yameandikwa na Matukio Daima Media 


Karibu kutembelea tovuti yetu www.MatukioDaimaHabari.co.tz au Youtube :Matukio Daima Tv 

  kwa ushauri piga 0754026299

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI