Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Zaina Mlawa akiwa na mstahiki meya Ibrahim Ngwada
HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa imeongoza katika makusanyo ya kodi ya ardhi katika Mkoa wa Iringa baada ya kukusanya Shilingi 1,106,801,243, ikiwa ni sehemu ya jumla ya Shilingi 2,979,601,789 zilizokusanywa na sekta ya ardhi mkoani humo hadi kufikia sasa.
Akizungumza leo katika kikao kazi cha Maafisa Ardhi wa Mkoa wa Iringa, Afisa Ardhi Mteule wa Mkoa huo, Christopher Ntenywa, alisema makusanyo hayo yanafikia asilimia 61 ya lengo la mwaka wa fedha 2025/2026 lililowekwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kwa mujibu wa Ntenywa, Halmashauri ya Mji wa Mafinga imekusanya Shilingi 687,853,141 na kushika nafasi ya pili, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa iliyokusanya Shilingi 313,698,678.
Alisema Halmashauri za Wilaya za Kilolo na Mufindi kila moja imekusanya Shilingi 204,382,199, huku Ofisi ya Ardhi Mkoa ikikusanya Shilingi 437,282,007 na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yakikusanya Shilingi 24,743,000.
Ntenywa alisema mafanikio hayo yanadhihirisha kuimarika kwa usimamizi wa mapato ya ardhi pamoja na mwitikio mzuri wa wananchi katika kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi ya ardhi.
Katika hatua nyingine, alisema kliniki 16 za ardhi zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa usajili wa hati milki, ambapo hati milki 2,513 kati ya hati 4,456 zilizosajiliwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 zilitokana na huduma zilizotolewa kupitia kliniki hizo.
Alibainisha kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na utekelezaji wa kampeni ya Samia Ardhi Kliniki, ambayo imeongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya umiliki wa ardhi, umuhimu wa kusajili ardhi na kupata hati milki.
“Kuendelea kufanyika kwa kliniki za ardhi kumesaidia kuondoa changamoto mbalimbali za ardhi kwa wananchi na kuongeza kasi ya utoaji wa hati milki, jambo linalochangia usalama wa umiliki wa ardhi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisema Ntenywa.
Akizungumzia kikao kazi hicho kamishna msaidizi wa Ardhi mkoa wa Iringa Rehema Kilonzi alisema kikao hicho ni sehemu ya maelekezo ya katibu mkuu wa wizara ya Ardhi ,Nyumba na maendeleo ya Makazi chenye lengo la kukumbushana majukumu ya kujipanga kuongeza ufanisi wa kazi .
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika programu za elimu ya ardhi na kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi ya ardhi kwa wakati ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za sekta hiyo.












0 Comments