Header Ads Widget

KAMATI YA ULINZI NA USALAMA KISARAWE YATOA NOTISI KWA WAFUGAJI WALIOVAMIA MSITU WA RUVU KUSINI


Na Mwandishi Wetu, Kisarawe


Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kisarawe imeendesha operesheni maalumu ya kutoa notisi kwa wafugaji wanaodaiwa kuvamia Hifadhi ya Msitu wa Ruvu Kusini, huku ikiwataka kuondoka katika eneo hilo kabla ya Julai 1, 2026.

Operesheni hiyo iliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Petro Magoti, na kushirikisha Jeshi la Polisi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Afisa Mifugo wa Wilaya pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri.

Katika operesheni hiyo iliyofanyika Juni 18, 2026, zaidi ya mazizi 12 yalitembelewa na wahusika kupewa notisi za kuondoka ndani ya hifadhi. Mazizi yaliyobainika kutokuwa na wafugaji wala mifugo yaliondolewa katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Mhe. Magoti alisema uvamizi wa maeneo ya hifadhi kwa shughuli za kibinadamu ni kinyume cha sheria na unatishia juhudi za Serikali za kulinda rasilimali za misitu na mazingira.

Aliwataka wananchi kuacha mara moja shughuli zote zisizoidhinishwa ndani ya hifadhi na kuheshimu mipaka ya maeneo yaliyohifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wafugaji wote waliopo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Ruvu Kusini kuhama kabla ya Julai 1, 2026, akionya kuwa baada ya muda huo Serikali itaanza operesheni ya kuwakamata wafugaji watakaobaki pamoja na mifugo yao.

Alisema hatua hizo zinalenga kulinda uhai wa hifadhi, kuzuia uharibifu wa mazingira na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI