Header Ads Widget

KAMATI YA BUNGE YAKUTANA NA WIZARA YA KUJADILI NJIA ZA KUIMARISHA SEKTA YA UTALII NA UHIFADHI


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekutana na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi pamoja na Wizara ya Fedha kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha masuala ya uhifadhi na sekta ya utalii nchini ili kuhakikisha sekta hizo zinakuwa na tija na manufaa kwa wananchi

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Timotheo Paul Mzava (Mb.), amesema maafisa wa uhifadhi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wanapaswa kwenda uwandani kufanya tathmini ya kina ya hali ya mapori Tengefu nchini ili kuhakikisha ustawi wa uhifadhi na maisha ya wananchi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Aidha, Mhe. Mzava amesema wizara hiyo inapaswa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Fedha, ili kuhakikisha wananchi wanapata stahiki zao za kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi wanaopata madhara kutokana na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu. 

Katika kukuza sekta ya utalii, Mhe. Mzava amesema ni muhimu kuendeleza mikakati mbalimbali, hususan kuvutia watalii kutoka Bara la Asia ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ya nchi.

“Ni muhimu kuhakikisha mikakati ya utalii inaendelezwa, hususan ule mkakati (Go East) wa kuvutia watalii kutoka Bara la Asia,” amesema Mhe. Mzava.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amesema wizara imeendelea kuongeza juhudi za kuimarisha uhifadhi nchini ili kuhakikisha rasilimali hizo zinalindwa na kutumika kwa manufaa ya Taifa.

Amesema juhudi hizo zinaendana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ni Mhifadhi namba moja katika kusimamia na kulinda rasilimali za maliasili kwa maslahi mapana ya Taifa.

Kikao hicho kimefanyika Bungeni jijini Dodoma na kimehudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Nkoba Mabula na viongozi wengine kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo TANAPA, TAWA, NCAA, TFS na TTB.
















Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI