Na Calvin Katera - Arusha.
Shirika la ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mei 5, 2026 limeendesha mafunzo maalum kwa watumishi wake kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na utoaji wa huduma ya kwanza (First Aid).
Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uadilifu, uwajibikaji na uwezo wa watumishi kushughulikia dharura mbalimbali wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku pia wamekumbushwa umuhimu wa kuzingatia maadili ya kazi, kuepuka vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Maria Kirombo Saidia akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi CPA Musa Nasoro Kuji. Kamishna Kirombo alisisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia maadili ya kazi, nidhamu na uadilifu katika kuwahudumia wananchi na wageni wanaotembelea hifadhi za taifa.
Aidha Alieleza kuwa mafunzo ya huduma ya kwanza yanawawezesha watumishi kuwa tayari kukabiliana na dharura, kuokoa maisha na kutoa msaada wa haraka kwa wageni na wananchi wanaotembelea hifadhi za taifa.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Red Cross, Bi. Dora Samson, alielezea umuhimu wa TANAPA kupata mafunzo ya huduma ya kwanza, akibainisha kuwa watumishi wanapaswa kuwa na ujuzi wa msingi wa kukabiliana na dharura ili kuokoa maisha na kutoa msaada wa haraka pindi ajali au changamoto za kiafya zinapotokea ndani ya hifadhi.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka TAKUKURU Bw. Sifaeli Mshana alisisitiza haja ya kukomesha vitendo vya rushwa, hususan vinavyoweza kuwaathiri wageni, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaharibu taswira ya nchi na sekta ya utalii kwa ujumla. Kadhalika aliwataka watumishi wote kuwa mabalozi wa uadilifu na kuhakikisha wanatoa huduma kwa haki na usawa.
Mafunzo haya ni moja ya mkakati wa Shirika kuelekea mashindano ya AFCON 2027, ambapo ongezeko la wageni linatarajiwa.
TANAPA inalenga kuhakikisha wageni wote watakaotembea maeneo ya Hifadhi za Taifa wanapatiwa huduma bora, salama na yenye weledi wa hali ya juu.


















0 Comments