NA HADIJA OMARY
LINDI.......Wakati msimu wa mauzo ya mazao ya Wakulima 2026, ukikaribia kuanza Wakala wa Vipimo Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Kampuni ya Rotai na Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, wamezindua rasmi zoezi la uhakiki na matengenezo ya mizani za kidijitali
Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi za Chama cha Msingi Kitumiki AMCOS, Manispaa ya Lindi, ukihudhuriwa na viongozi wa vyama vya ushirika, wakulima na wataalamu wa vipimo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Vipimo aliyemwakilisha Meneja wa Mkoa wa Lindi, Selemani Jandwa, alisema kuwa jukumu lao la msingi ni kuhakikisha mizani zote zinazotumika katika ununuzi wa mazao zinakuwa katika viwango vinavyotakiwa kisheria.
“Msimu wa mazao ukikaribia ni muhimu mizani zote ziwe sahihi. Hatutaki mkulima apunjwe kwa sababu ya mzani mbovu. Ndiyo maana tunashirikiana na Kampuni ya Rotai kufanya matengenezo pindi dosari zinapobainika,” alisema Jandwa.
Kwa upande wake, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Lindi, Kenneth Shemdoe, alifafanua kuwa matumizi hayo ya mizani za kidijitali yametokana na maelekezo ya Serikali kupitia Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika nchini.
Alisema Mrajisi Mkuu ameagiza vyama vyote vya msingi vinavyojihusisha na mazao kupima mazao hayo kwa kutumia mizani za kidijitali pekee.
“Sisi kama Idara ya Ushirika Mkoa wa Lindi tuko tayari kusimamia kwa ukamilifu matumizi hayo. Hatutakubali mzani wa mkono uendelee kutumika na kuendeleza wizi kwa wakulima wetu,” alisisitiza Shemdoe.
Wakulima waliohudhuria hafla hiyo wameipongeza hatua hiyo, wakisema kuwa mizani za kidijitali zimekuja kuwaokoa na udanganyifu wa muda mrefu.
“Zamani tulikuwa tunaibiwa sana. Mzani wa mkono unachezewa, lakini sasa hivi mzani wa kidijitali ukikupima, risiti inatoka na SMS inaingia kwenye simu yako papo hapo. Haki inaonekana,” alisema Hamisi Chilinga Mwenyekiti wa chama cha msingi kitumiki AMCOS
Bakari Rashidi- , mkulima na mwanachama wa chama cha msingi kitumiki AMCOS, aliongeza kuwa mfumo huo mpya unawapa amani na uhakika. “Sasa hata nikilala nina uhakika kuwa kilo nilizouza ndizo zilizolipwa. Hakuna mtu ataniambia ‘mzani uliharibika’. Kila kitu kiko wazi na kimeandikwa,” alisema huku akitabasamu.
Hatua hiyo ya kuanza kutumia mizani za kidijitali inatajwa kuwa sehemu ya maandalizi mapema ya Mkoa wa Lindi kuelekea msimu wa mazao wa mwaka 2026, huku lengo likiwa ni kuhakikisha mkulima anapata haki yake na kuondoa kabisa malalamiko ya upungufu wa vipimo yaliyokuwa yakijitokeza kila msimu.

.jpeg)

.jpeg)





0 Comments