Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera
Mkuu wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Erasto Yohana Sima, amewataka wakulima wa kahawa kuzingatia ubora wa kahawa yao wakati wa uvunaji na utunzaji wa mazao yao ili kuweza kuongeza mnyororo wa thamani sokoni na kupata bei nzuri.
DC Sima amesema hayo hivi karibuni katika mkutano wa 36 wa chama kikuu cha ushirika cha KCU 1990 Ltd, ambapo ameeleza kuwa ubora wa kahawa utasaidia mkulima kupata kupata bei nzuri na kupanda kwa thamani ya kahawa katika soko la Dunia.
"kama mnavyojua serikali imekuwa ikisisitiza suala la ubora wa kahawa, suala la ubora wa kahawa halina mbadala kwani kahawa safi inasaidia kupata bei nzuri sokoni, niwahase vyama vya ushirika na msingi kuwasimamia wakulima kutozalisha kahawa chafu na isiyokomaa"
Aidha mkuu huyo wa wilaya amevitaka vyama vya ushirika na msingi kutumia tehama na mizani ya kidigitali ili kutomdhurumu mkulima wakati wa upimaji wa kahwa yake na kupata kile anachostahili.
"nisistize pia suala la tehama na mizani ya kidigitali serikali imesambaza mizani hiyo ili kuhakikisha mkulima hamnyonyi wakati wa upimaji kahawa yake"
Akiwasilisha rasmu ya bajeti na makisio kwa mwaka 2026/2027 mhasibu wa chama hicho Tatianis Kamoi alieleza kuwa wanatarajia kukusanya tani elfu 12 za kahawa na wanalenga kuuza katika soko la ulaya na bara la Asia.
"katika msimu wa kahawa wa 2026/27 tunatarajia kukusanya kilo 10,000,000 za kahawa ya kawaida na Organic kilo 2,500,000 kahawa safi tukilenga kuuza katika soko la ulaya na soko jipya la India"
Naye Mwenyekiti wa bodi ya KCU 1990 Lmtd, Ready Mashelano amesema kuwa katika mwaka ujao wa 2026/2027 wanatarajia kuongeza vitega uchumi ili kuongeza mapato ya chama hicho na pia wanalenga kuvisaidia vyama vya msingi AMCOS na wakulima kwa kujenga duka la pembejeo.
"tunatarajia kukamilisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano, ukarabati wa benki ya wakulima kwa shilingi million 283, na tunatarajia kuanza utekelezaji wa ujenzi wa hotel ya like kwa shilingi milioni 557 na tunatarajia kuanza ujenzi wa duka kubwa la pembejeo litakalogharimu shilingi milioni 703"
Nao baadhi ya wajumbe wa mkutano huo akiwemo Respicius John ameitaka bodi ya chama hicho kuvikumbuka vyama msingi (AMCOS) na wakulima kwa kuwapatia faida zinazotokana na vitega uchumi vya chama hicho kwani AMCOS na wakulima ndio wachangia wakuu wa mapato ya chama hicho.
"tunahitaji hata vyama hivi vya msingi AMCOS kupate faida kutokana na mapato ya hivi vitega uchumi vya ushirika kwa sababu wakulima na AMCOS ndio wachangia wakubwa wa mapato ya ushirika tugawane kidogo hayo mapato yashukwe kwenye AMCOS"
Katika mwaka wa 2026/2027 chama kikuu cha ushirika KCU 1990 Lmtd kichojumuisha wilaya za Missenyi, Muleba na Bukoba kinatarajia kukusanya na kutumia zaidi ya shilingi bilioni 2.6 zitazotokana na mauzo ya kahawa, vitega uchumi vya ushirika na mikopo.


.jpeg)
.jpeg)






0 Comments