Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Arusha.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewataka waandishi wa habari nchini kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi ili kuepuka kushawishiwa na wanasiasa wasio waadilifu pamoja na wala rushwa.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa kufunga maadhimisho kuelekea Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Makonda alisema uhuru wa habari hauwezi kuwa kamili bila uhuru wa kiuchumi kwa wanahabari.
Alisema baadhi ya waandishi wamekuwa wakiandika habari kwa maslahi ya wanasiasa, hali ambayo ni hatari kwa mustakabali wa taaluma ya habari na inaweza kupotosha jamii.
“Ni muhimu kwa mwandishi wa habari kuwa na uhuru wa kiuchumi ili aweze kufanya kazi yake bila hofu, upendeleo au shinikizo kutoka kwa watu wenye maslahi binafsi,” amesema Makonda.
Ameongeza kuwa kuna watu wasiokuwa waaminifu wanaowashawishi waandishi kwa maslahi yao, na kusisitiza umuhimu wa wanahabari kuzingatia maadili ya taaluma yao pamoja na kuandika habari zinazojenga taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri Makonda ameagiza kuundwa kwa timu ya wanahabari kwa kushirikiana na wizara ili kuhakikisha mapendekezo 15 yaliyowasilishwa yanapelekwa bungeni na kujadiliwa.
Akizungumzia Dira ya Taifa 2050, amesema wanahabari wanapaswa kuwa chachu ya maendeleo kwa kutoa taarifa sahihi na kuhamasisha jamii kushiriki katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Tech & Media Convergence (TMC), Asha Abinallah, aliwasilisha mapendekezo 15 akisisitiza umuhimu wa kulinda usalama wa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, hasa wanapokumbana na mazingira hatarishi.
Naye mwakilishi kutoka UNESCO, Michael Toto, amesema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa wadau wa sekta ya habari kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika kuimarisha demokrasia, uwajibikaji, maendeleo endelevu na amani.
Ameongeza kuwa UNESCO itaendelea kuunga mkono sekta ya habari huku akiwahimiza waandishi kuandika habari za ukweli pamoja na kupinga ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
Katika maadhimisho hayo Chama cha waandishi wa Habari vijijini (RUJAT) kimewakilishwa na viongozi wa kamati tendaji kwa ufadhili wa kampuni ya MATI Foundation ya mkoani Manyara ambayo inahamasisha ushiriki wa vyombo vya habari katika kuhamasisha uwekezaji wa ndani kwa mstakabali wa uchumi wa taifa.
Mwisho


.jpeg)
.jpeg)





0 Comments