Header Ads Widget

TANZANIA NA BELARUS KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA BANDARI

Tanzania na Belarus zimeazimia kuimarisha ushirikiano katika sekta ya bandari, hatua inayolenga kukuza uchumi na kuongeza fursa za kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Mheshimiwa Maxim Ryzhenkov, alipotembelea makao makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) jijini Dar es Salaam tarehe 29 Aprili 2026, na kujionea shughuli mbalimbali za bandari.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Dkt. Baraka Mdima, amesema mamlaka hiyo iko tayari kushirikiana na Belarus katika kuboresha usafirishaji wa mazao ya kilimo, hasa yale yanayoharibika kwa haraka.

Ameeleza kuwa TPA inaendelea kuboresha miundombinu ya kisasa ya bandari pamoja na kuandaa maeneo maalum kwa ajili ya kuhudumia shehena za mazao hayo, akitaja Bandari ya Tanga na Bandari ya Bagamoyo kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yatakayochangia juhudi hizo.

Kwa upande wake, Mhe. Ryzhenkov amesema Belarus imevutiwa na maendeleo ya bandari za Tanzania na iko tayari kuitumia Tanzania kama lango la kusafirisha mazao yake ya kilimo kwenda masoko ya kimataifa.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Mhe. Fredrick Kibuta, amepongeza hatua hiyo, akibainisha kuwa ushirikiano huo utafungua fursa mpya za biashara na uwekezaji, sambamba na kuboresha usafirishaji wa bidhaa, hususan mazao ya kilimo, kupitia bandari za Tanzania kuelekea masoko ya kimataifa.




 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI