Na Hamida Ramadhan Arusha
MWENYEKITI wa Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT), Neville Meena, amesema kuwa ni muhimu kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari huku ikiwekewa mkazo sauti ya wananchi wa vijijini ili kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma katika upatikanaji wa taarifa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika jijini Arusha, Meena amesema uhuru wa vyombo vya habari unapaswa kuambatana na uwajibikaji wa kitaaluma kwa wanahabari kuzingatia misingi ya ukweli, usahihi, uwiano na maslahi ya umma.
Maadhimisho hayo yaliyowakutanisha wadau wa sekta ya habari kwa siku mbili katika Hoteli ya Mount Meru, yalijadili mustakabali wa tasnia ya habari katika muktadha wa mabadiliko ya kidijitali, yakilenga pia kukuza ubunifu na kuhakikisha uendelevu wa taaluma ya uandishi wa habari.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa RUJAT, Prosper Kwigize, amesema chama hicho kimejipanga kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo MCT, MISA, UTPC, UNESCO, TAMWA na TADIO ili kubadili mwelekeo wa uandishi wa habari unaojikita zaidi mijini.
Amesema wananchi wa vijijini mara nyingi huathirika zaidi katika changamoto za amani na usalama, lakini bado wanakosa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika habari kutokana na changamoto za miundombinu ya mawasiliano na uwekezaji mdogo katika maeneo hayo.
Aidha, RUJAT imeipokea kwa shukrani kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuhusu kuundwa kwa kamati ya pamoja kati ya wadau wa habari na Wizara ili kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya mkutano huo.









0 Comments