Na Fadhili Abdallah,Kigoma
SERIKALI ya Tanzani imeifunga rasmi kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi kwa zaidi ya miaka 10 huku Waziri wa mambo ya Ndani Patrobas Katambi akihimiza umuhimu wa kutunza amani ya nchii yetu.
Akizungumza katika hafla ya kufungwa kwa kambi hiyo ya Wakimbizi waziri Katambi alisema kuwa uwepo wa wakimbizi wa Burundi waliokuwa wakihifadhiwa kwenye kambi hiyo ni kielelezo halisi cha kuvurugika kwa Amani katika nchi yao na hivyo raia hao wa Burundi hawakuwa na chaguo lingine Zaidi ya kukimbia nchi yao na kuomba hifadhi katika nchi nyingine.
Kutokana na hilo alitoa wito kwa watanzania kulinda na kudumisha Amani ya nchi yetu kwani Amani hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya Watanzania na kwamba kutoweka kwa Amani kutasababisha shughuli zote za maendeleo na mambo muhimu ambayo watanzania walijipangia hawataweza kuyafanya.
Pamoja na kurudishwa kwa wakimbizi hao Waziri Katambi alisema kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu kulinda sheria za kimataifa ambazo imeridhia sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Naibu Mkuu wa UNHCR nchini, Zulqarnain Hussain ANJUM ameishukuru Tanzania kwa moyo wake wa ukarimu wa kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi hao ambao waliishi kwa Amani na usalama muda wote hadi wanarudhishwa nchini kwao.
Awali Mkurugenzi wa idara ya Wakimbizi ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi, Sudi Mwakibasi alisema kuwa Tanzania ilianza kuwahifadhi wakimbizi wa Burundi katika kambi hiyo mwaka 2016 wakipokea jumla ya wakimbizi 127,000 na hadi kambi inafungwa jumla ya wakimbizi Zaidi ya 166,330 walikuwa wamerejeshwa Burundi.
Mwakibasi alisema kuwa kambi hiyo ilikuwa ifungwe Machi 31 mwaka huu lakini iliongezewa mwezi mmoja hadi kufikia April 30 baada ya kuwepo kwa wakimbizi waliojitokeza nje ya utaratibu lakini walisaidiwa na kurudishwa nchini kwao na kwa sasa mpango wa urejeshaji unahamia kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya kasulu mkoani Kigoma ambapo hadi kufikia Juni 30 wakimbizi wa Burundi katika kambi hiyo wanatakiwa wawe wamerudishwa nchini kwao na hivyo kambi hiyo kubaki na wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pekee.


.jpg)






0 Comments