Na Matukio Daima, Media Morogoro
BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kwa kushirikiana na wahasibu na wakaguzi kutoka maeneo mbalimbali nchini, imetoa msaada katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ukiwemo ulipaji wa gharama za matibabu kwa baadhi ya wagonjwa, uchangiaji damu pamoja na vifaa tiba.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi, amesema hatua hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za sekta ya afya na kusaidia makundi yenye uhitaji, hususan watoto na kina mama.
Amesema bado kuna umuhimu wa taasisi na jamii kushiriki katika kusaidia huduma za kijamii badala ya kuacha jukumu hilo kwa Serikali pekee.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Baraza la Rufani za Kodi, CPA Sura Sabas Kimboka, amesema wameguswa na mahitaji yaliyopo kwenye jamii kwa sababu na wao ni sehemu yake ndio maana wakaamua kutoa mahitaji hayo.
Akatoa wito kwa Taasisi nyingine kujitokeza kusaidia wahitaji, akisisitiza kuwa watoto na kina mama hasa wajawazito wanahitaji msaada wa haraka wanapokumbwa na changamoto za kiafya.
Akizungumzia msaada huo kwaniaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Mratibu wa Huduma za Tiba, Dkt. Azael Kyando, ameshukuru kwa msaada huo na kueleza umekuja wakati muafaka.
Amesema hospitali hiyo inapokea wagonjwa wengi, lakini baadhi yao hushindwa kumudu gharama za matibabu, hali inayoweza kuchelewesha upatikanaji wa huduma.
Akaongeza kuwa ushirikiano wa wadau kama NBAA ni muhimu katika kusaidia makundi yenye uhitaji na kuboresha utoaji wa huduma za afya sio tu kwa hospitali hiyo lakini hata kwa maeneo mengine.








0 Comments