Header Ads Widget

WADAU WA UTATU WAAFIKI KUIMARISHA SEKTA YA KAZI NA AJIRA


Na: OWM (KAM) - Dodoma

Wadau wa Utatu ambao ni Serikali, Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Vyama vya Waajiri (ATE) wamekutana na kufanya majadiliano yaliyolenga kuimarisha ushirikiano katika kuendelea kuimarisha sekta ya kazi na ajira nchini kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Taifa na kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Kikao hicho cha pili cha Kamati ya Majadiliano baina ya Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Waajiri, kilichofanyika Aprili 17, 2026 jijini Dodoma, ambapo kilifunguliwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu.

Akifungua kikao hicho, Mhe. Sangu alisisitiza kuwa ushirikiano wa wadau hao utazingatia maslahi mapana ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii, huku akihimiza kuendelezwa kwa umoja na mshikamano ili kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa.

Aidha majadiliano hayo yamejikita katika kuweka misingi imara ya usimamizi wa sekta ya kazi na ajira nchini, ikiwemo kuimarisha mazingira ya kisheria, kisera na kiutawala, pamoja na kuhakikisha haki, usawa na uwajibikaji vinazingatiwa kwa pande zote. Aidha, msisitizo umewekwa katika kuwajengea wafanyakazi nidhamu ya kazi, weledi na utii wa sheria za nchi ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Vilevile, wadau hao wamejadili umuhimu wa kuheshimu haki za wafanyakazi na utekelezaji wa mikataba ya kazi, wakitambua kuwa rasilimali watu ni mhimili muhimu wa mafanikio ya kiuchumi. Hivyo, wamekubaliana kuendelea kukuza mazingira bora ya kazi yenye staha, usalama na motisha yatakayochochea ubunifu, ushindani na tija endelevu.

Kwa upande wa Serikali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Mary Maganga, amewashukuru wadau wa Utatu ikiwemo TUCTA na ATE kwa ushiriki wao na ushirikiano mzuri unaoendelea kuimarisha utekelezaji wa masuala ya sekta ya kazi na ajira nchini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATE Bi. Susan Ndomba, ameipongeza Serikali kwa kuendeleza ushirikiano huo, akibainisha kuwa mshikamano wa wadau wa Utatu unawezesha kushughulikia changamoto mbalimbali kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Rais wa TUCTA Bw. Tumaini Nyamhokya, ametoa shukrani kwa wadau wote wa Utatu kwa kuendeleza ushirikiano imara, akisisitiza kuwa umoja huo ni chachu muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa ya Dira ya mwaka 2050.
MWISHO.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI