Header Ads Widget

DKT. KESSY ACHUKUA USUKANI KUONGOZA - TANAPA KANDA YA KASKAZINI



Na Calvin Katera - Arusha


Wakati dunia ikisisitiza usawa katika nafasi za uongozi kwa wanawake, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limendelea kushika hatamu kwa kuwaamini na kuwapa wanawake nafasi za juu katika uongozi.

Hatua hii imejidhihirisha katika bandika bandua au kata mti panda mti baada ya aliyekuwa Mkuu wa Kanda ya Kaskazini (mst) Mwanamke, Naibu Kamishna Steria ndaga kukabidhi kijiti cha uongozi kwa mwanamke mwenzie Kamishna Msaidizi Mwandamizi Dkt. Beatrice Kessy katika hafla fupi iliyofanyika Makao Makuu ya Kanda ya Kaskazini yaliyopo Majengo Arusha leo Aprili 14, 2026.

Akikabidhi Kanda hiyo yenye hifadhi 5 Kamishna Ndaga alisema kuwa watumishi wa kanda ni wenye ushirikiano, nidhamu, weledi na wasiosukumwa katika utekelezaji wa majukumu hasa pale kila mmoja ananapotimiza wajibu wake. 

"Naondoka nakuachia ofisi iliyojaa watumishi wenye ushirikiano, kiu ya maendeleo na tuliofanya nao kazi bila kusukumana na kujenga msingi wa mafanikio ya pamoja ambayo leo yanatupa sifa ndani ya kanda yetu ya kaskazini" Alisema Naibu Kamishna Ndaga.

Akipokea kijiti hicho Dkt. Kessy alisema anaahidi kushirikiana na watumishi kuhakikisha hifadhi za kaskazini zinaimarisha uhifadhi huku zikishika kidedea katika makusanyo ya mapato, kutangaza utalii na vivutio sambamba na uboreshwaji wa miundombinu ya hifadhi.

"Ushirikiano huu mliouonesha awali na udumishwe zaidi ili kuboresha mazingira rafiki ndani ya hifadhi zetu tano za kanda hii kuwa vinara wa ukusanyaji mapato, utalii na miundombinu ambapo tutapata fursa ya kuwavutia wageni wengi na kujinyakulia tuzo katika anga za kitaifa na kimataifa" alisema Kamishna Dkt. Kessy.

Katika utumishi wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga Mkuu wa Kanda Mstaafu ametumikia TANAPA tangu mnamo mwaka 1995  katika Hifadhi mbalimbali za Taifa ikiwemo Udzungwa, Ziwa Manyara, Arusha na Rubondo na baadae kutunukiwa Cheo cha Unaibu Kamishna na kutumikia kanda tatu ikiwemo Mashariki, Kusini na Kaskazini.










Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI