Header Ads Widget

ZAIDI YA VIJANA 4,000 WAJISAJILI BUNGE MARATHON 2026

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

ZAIDI ya vijana 4,000 wamejisajili kushiriki mbio za Bunge Marathon zinazotarajiwa kufanyika Aprili 18, 2026 katika Uwanja wa Jamhuri, huku maandalizi ya tukio hilo yakikamilika kwa zaidi ya asilimia 100.



Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Bunge Marathon, Festo Sanga, alisema kuwa huu ni msimu wa tatu wa mbio hizo ambazo zimeendelea kukua kwa kasi na kuvutia washiriki wengi zaidi kila mwaka.


Amesema wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Silent Ocean, wamehakikisha maandalizi yote muhimu yanakamilika kwa wakati, ikiwemo upatikanaji wa vifaa na uratibu wa vituo vya usajili katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Sanga, hadi kufikia sasa zaidi ya washiriki 4,600 wamejisajili, huku idadi kubwa ikiwa ni vijana, jambo linaloashiria mwitikio mkubwa wa kizazi kipya katika kushiriki michezo na shughuli za kijamii.


Mbio hizo zitahusisha umbali wa kilomita 5, 10, 15 na 21, ambapo washiriki wote watapatiwa medali, huku washindi wakijinyakulia zawadi mbalimbali za fedha taslimu.

Katika mbio za kilomita 5, mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 2, wa pili shilingi 1,000,000 na wa tatu shilingi 500,000, huku washika nafasi ya nne hadi ya kumi nao wakipata zawadi.


Kwa upande wa kilomita 10 na 21, mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 6, wa pili milioni 3 na wa tatu milioni 1.5.

Aidha, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Rogath Akhwar, amesema mashindano ya mwaka huu yamepandishwa hadhi na kufikia kiwango cha kimataifa, huku nchi mbalimbali zikialikwa na baadhi ya washiriki wa kimataifa wakianza kujisajili.


 Waandaaji wa tukio hilo Silent Occean wamewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki, wakisisitiza kuwa Bunge Marathon ni riadha ya Watanzania wote inayolenga kuimarisha afya na kuimarisha uhusiano kati ya Bunge na wananchi.

Hata hivyo Mgeni rasmi katika mbio hizo anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI