Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, leo tarehe 1 Aprili 2026, amekabidhi rasmi gari aina ya "Coaster" kwa kikundi cha Madereva na Makondakta wa Mkata, ikiwa ni sehemu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, ikishirikisha viongozi mbalimbali wa wilaya na wanachama wa kikundi hicho.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, DC Nyamwese aliwapongeza vijana hao kwa kuonyesha umoja wa dhati na kuwahimiza kufanya kazi kwa bidi ili kutimiza lengo la kurejesha mkopo huo kwa wakati. "Nawapongeza kwa hatua hii, huu ni mfano wa vijana wanaojitambua.
Fanyeni kazi kwa bidii na hakikisheni mnatenga fedha za matengenezo ya gari hili mara kwa mara ili liweze kudumu na kuwasaidia katika shughuli zenu za kila siku," alisema Nyamwese.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Ndg. Saitoti Stephen, aliwataka vijana hao kuwa kielelezo cha uaminifu kwa vikundi vingine kwa kuzingatia nidhamu ya kazi na marejesho ya mikopo."Tunataka muwe mano wa kuigwa, ili vijana wengine nao waone inawezekana kupata mkopo na kujikwamua kiuchumi" alisisitiza Saitoti. Naye Mkuu wa ldara ya Mandeleo ya Jamii Wilaya ya Handeni, Bi. Rachel Mbelwa, alibainisha kuwa mradi huo una thamani ya shilingi milioni 90.
Alisema fedha hizo zimetolewa mahususi kwa ununuzi wa gari hilo ili kuwakwamua kiuchumi vijana hao na familia zao. Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa kikundi hicho cha Madereva na Makondakta wa Mkata, Majidi Amiri Mseza, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sera rafiki za uwezeshaji wananchi.
"Tunawashukuru viongozi wetu wa wilaya kwa kutuamini. Mkopo huu ni mkombozi kwetu na tunahaidi kuwa mabalozi wazuri kwa vijana wengine ili nao waone umuhimu wa kujiunga katika vikundi na kunufaika na mikopo hii ya asilimia 10," alisema Mseza.








0 Comments