Header Ads Widget

BIASHARA YA MAGODORO CHAKAVU YASHIKA KASI DAR, WATAALAM WAONYA MADHARA YAKE KIAFYA

 


Na Matukio Daima Media

Wakati wakazi wengi wa mabondeni jijini Dar es Salaam wakiendelea kuhesabu hasara baada ya mali zao kuharibiwa na mafuriko, kwa baadhi ya wajasiriamali hali hiyo imegeuka kuwa fursa mpya ya biashara kupitia ukusanyaji na uuzaji wa magodoro chakavu.

Uchunguzi uliofanywa na Matukio Daima Media umebaini kuwa shehena ya magodoro chakavu hukusanywa katika maeneo mbalimbali ya jiji kabla ya kusafirishwa kwenda mikoani. Baadhi ya magodoro hayo yameonekana katika eneo la Stendi ya Mbezi kwa Yusuph, yakipakiwa kwenye magari tayari kwa safari ya kwenda kuuzwa katika mikoa tofauti.

Mmoja wa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hiyo, Khamis Juma, amesema magodoro mengi hupatikana baada ya wakazi kuyatupa kufuatia kuharibiwa na maji ya mafuriko.

Alisema wao hununua magodoro hayo kwa bei ndogo, kisha huyafanyia marekebisho kwa kuweka flonya (kitambaa kipya cha nje) ili yaonekane kama mapya kabla ya kuyauza tena sokoni.

“Tunauza godoro moja kati ya Sh75,000 hadi Sh100,000 kutegemea na ukubwa wake,” alisema.

Khamis alieleza kuwa kwa kawaida hununua godoro moja kwa kati ya Sh15,000 hadi Sh20,000, huku mengine wakiyapata bure baada ya wahusika kuyatupa.


Halima Omary na Alex Johnson wakazi wa Kinyerezi Jijini Dar es Salaam walisema kwa upande wao wamekuwa wakilazimika kukusanya madogoro hayo toka kwa wahanga wa mafuriko na kuwalipa kati ya Tsh 10,000 hadi 15000 kisha wao huuza kwa walanguzi hao ambao wamekuwa wakiwao geza Tsh 5000 zaidi kwa kila Godoro moja .


Huku Sarah Frank mkazi wa Tandele alisema wao kama wahanga wa maji kuharibu mali zao wamekuwa wakiuza ama kuyagawa bure magodoro hayo maana hayana kazi tena .

Hata hivyo, licha ya biashara hiyo kuonekana kuwa na faida kwa baadhi ya wafanyabiashara, wataalamu wa afya wanaonya kuwa matumizi ya magodoro chakavu yaliyolowa maji au yaliyochakaa yanaweza kusababisha matatizo mbalimbali ya kiafya kwa watumiaji.


Madhara ya Kiafya Yanayoweza Kujitokeza Magonjwa ya ngozi

DKT John Ndalimalo anasema kuwa Magodoro yaliyolowa maji kwa muda mrefu yanaweza kukuza fangasi na bakteria wanaoweza kusababisha magonjwa ya ngozi kama upele, kuwashwa au vidonda.

Magonjwa ya mfumo wa hewa Vumbi, ukungu na wadudu wadogo (dust mites) wanaoweza kujificha kwenye magodoro chakavu wanaweza kusababisha mzio, mafua sugu, pumu na matatizo ya kupumua.

Maambukizi ya bakteria Magodoro yaliyotumika na watu wengine bila kusafishwa vizuri yanaweza kubeba bakteria au vijidudu vinavyoweza kusababisha maambukizi ya kiafya.

Kuenea kwa kunguni na wadudu wengine Magodoro chakavu mara nyingi huwa na kunguni au wadudu wengine wanaosababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji na pia kuathiri afya ya ngozi.


Harufu na ukungu (mold) Magodoro yaliyolowa maji yanaweza kutoa harufu mbaya na kuota ukungu unaoweza kuwa hatari kwa afya, hasa kwa watoto na wazee.

Kutokana na hatari hizo, wataalamu wa afya wanashauri wananchi kuwa makini wanaponunua magodoro, kuhakikisha wanapata magodoro mapya au yaliyosafishwa kitaalamu, ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kiafya.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI