Serikali imependekeza hatua mbalimbali za kikodi zitakazolenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuharakisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira nchini katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Hatua hizo zimetangazwa leo Juni 11, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Miongoni mwa mapendekezo hayo, Serikali imependekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mita janja za gesi ya mitungi ya kupikia (LPG Smart Meter) zinazoingizwa nchini ili kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia katika ngazi ya kaya.
Aidha, Serikali imependekeza kuendelea kutoa vivutio mbalimbali vya kikodi katika sekta ya gesi na umeme ikiwemo msamaha wa kodi kwenye vifaa vinavyotumika kubadilisha magari kutoka mfumo wa matumizi ya mafuta kwenda matumizi ya gesi na umeme pamoja na vifaa vya miundombinu ya gesi.
Waziri Omar amesema hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala nchini huku ikipunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Serikali imependekeza kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa baadhi ya magari yanayotumia umeme pamoja na kusamehe kodi kwenye vifaa vinavyotumika katika vituo vya kuchaji magari hayo.
Hatua hizo zinatarajiwa kuongeza matumizi ya nishati safi katika sekta ya usafiri na majumbani, kupunguza gharama za matumizi ya nishati kwa wananchi na kuchangia juhudi za kuhifadhi mazingira sambamba na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.






0 Comments