RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir amemfuta kazi Spika wa Bunge la nchi hiyo, Jemma Nunu Kumba pamoja na Naibu wake, Permena Awerial Aluong, kupitia amri iliyosomwa bungeni Jumanne.
Tangazo hilo limetolewa Jumanne 6 Aprili 2026 na mkuu wa wabunge wa chama tawala cha Sudan People's Liberation Movement (SPLM), Tulio Odongi Ayahu, ambaye amesema uamuzi huo unawahusu viongozi hao wa Bunge la Mpito.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya wabunge wa SPLM kuwasilisha ombi la kumuondoa Kumba madarakani, wakimtuhumu kuhusika na vitendo vya rushwa vinavyohusiana na matumizi mabaya ya fedha za Bunge.
Kumba ambaye aliandika historia mwaka 2021 kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini Sudan Kusini, hajatoa majibu kuhusu tuhuma hizo mpaka sasa.
Baada ya mabadiliko hayo, Rais Kiir amemteua Joseph Ngere Paciko kuwa Spika mpya wa Bunge, huku Abuk Paiti Ayiik akichukua nafasi ya Naibu Spika.
Uamuzi huo unakuja ikiwa ni wiki chache tangu Rais Kiir alipomtimua ghafla Waziri wa Fedha, Bak Barnaba Chol, aliyekuwa madarakani kwa miezi mitatu pekee bila kueleza sababu.






0 Comments