Header Ads Widget

VIJANA IFAKARA WAPATA KAZI YA MATENGENEZO YA BARABARA YENYE THAMANI YA MILIONI 13.4 KUPITIA MPANGO WA CBRM



Ifakara

Katika kuendelea kutekeleza mpango wa ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za maendeleo, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mpango wa ushirikishwaji wa vikundi vya kijamii (CBRM) imekipatia kazi Kikundi cha Bodaboda kinachojulikana kama Milola Mificheni kilichopo Kata ya Kibaoni, Halmashauri ya Mji Ifakara.

Kikundi hicho cha vijana kimepata kazi ya matengenezo ya barabara yenye thamani ya Shilingi milioni 13.4, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuwainua vijana kiuchumi na kuwashirikisha moja kwa moja katika shughuli za maendeleo ya miundombinu ya barabara.

Kwa sasa kikundi hicho kimeanza kutekeleza kazi za matengenezo ya mara kwa mara, ikiwemo kufyeka nyasi katika barabara ya Kapolo–Nakafuru–Kibaoni yenye urefu wa kilomita 4.4, iliyopo Tarafa ya Ifakara.

Mpango wa ushirikishwaji wa vikundi vya kijamii katika matengenezo ya mara kwa mara ya barabara (CBRM) una lengo la kuongeza ajira kwa vijana, akina mama na watu wa rika mbalimbali kwenye vikundi vya kijamii huku ukichangia kuboresha hali ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mwaka wa fedha 2025/26, Mpango huo umeanza  katika Mikoa minne kwenye wilaya nane ikiwemo Tanga (Lushoto na Korogwe) Morogoro (Mvomero na Kilombero) Pwani (Rufiji na Mkuranga) pamoja na Dodoma (Kongwa) jumla ya vikundi 302 ambapo watu  zaidi ya 1500 watanufaika na mpango huo pia  barabara zenye urefu wa zaidi ya Km 1500 zinaboreshwa.

Aidha, kwa mwaka wa fedha  2026/27, Mpango huo unatarajiwa kutekelezwa nchi nzima katika Mikoa 25 kasoro Dar es salaam.

Utekelezaji huo utajumuisha zaidi ya Halmashauri 100 na zaidi ya Km. 7000 za barabara zitaboreka na inatarajiwa vikundi zaidi ya 1400 na watu zaidi ya 7200 watanufaika na mpango huu nchini.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI