Header Ads Widget

VIJANA JIKITENI KWENYE KILIMO CHA KISASA, KUPATA UJUZI - NW WANU

 


Na Lilian Kasenene, Morogoro

Matukio DaimaApp 

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kisasa katika sekta ya kilimo ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Ujasiriamali wa Vijana kwa Mustakabali wa Chakula na Kilimo (Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture-YEFFA) uliofanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA Kihonda, Morogoro, Naibu Waziri huyo alisema mradi huo unalenga kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo katika teknolojia za kilimo, umwagiliaji na uhifadhi wa mazao baada ya mavuno.

Alieleza kuwa matumizi sahihi ya teknolojia katika kilimo yataongeza uzalishaji wa mazao na kupunguza upotevu baada ya mavuno, jambo litakalosaidia kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Naibu Waziri Ameir pia alisisitiza kuwa serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuifanya kuwa ya kisasa na yenye tija zaidi.

Alibainisha kuwa sekta ya kilimo ni muhimu kwa uchumi wa taifa kwani inatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania.

Aidha, aliwataka vijana kutumia fursa zinazotolewa na miradi ya maendeleo kama YEFFA ili kujifunza ujuzi mpya, kuanzisha biashara za kilimo na kuchangia maendeleo ya taifa.

Alisema kuwa kwa kuwekeza katika elimu, teknolojia na ubunifu, vijana wataweza kuifanya sekta ya kilimo kuwa chanzo kikubwa cha ajira na maendeleo ya uchumi nchini.

“Ili sekta hii iweze kushindana kikanda na kimataifa, ni lazima iendelezwe na nguvu kazi yenye ubunifu, ujuzi na maarifa ya kibiashara. Katika kipindi cha sasa tunaona mabadiliko makubwa katika kilimo, kuanzia matumizi ya zana na mitambo ya kisasa,” alisema Ameir.

Aliongeza kuwa jumla ya vijana 5,631 kutoka mikoa 19 ya Tanzania Bara wanatarajiwa kunufaika na mafunzo kupitia mradi huo, huku vijana 762 tayari wakiwa wamepata mafunzo katika fani mbalimbali.

Alisema hiyo ni fursa muhimu kwa vijana na akawahimiza kuitumia ipasavyo ili kupata stadi zitakazowasaidia kufanya shughuli za ufundi wa zana za kilimo na kuimarisha uzalishaji.

“Kilimo cha leo si cha jembe la mkono pekee, bali ni kilimo cha teknolojia, thamani na biashara. Hivyo vijana wetu wanapaswa kuandaliwa kwa ujuzi unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani katika kilimo,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthony Kasore, alisema mradi huo umeanzishwa kwa kuzingatia changamoto ya ukosefu wa ajira na ajira zisizo rasmi kwa vijana, hususan wa vijijini.

Alisema changamoto hiyo inachangiwa na upungufu wa ujuzi wa vitendo unaoendana na mahitaji ya soko pamoja na teknolojia za kisasa za kilimo, hali inayosababisha tija ndogo na kipato kidogo kwa vijana wengi.

Aliongeza kuwa licha ya sekta ya kilimo kuwa na mchango mkubwa katika uchumi, bado inakabiliwa na changamoto za matumizi hafifu ya teknolojia, upotevu wa mazao baada ya mavuno na uhaba wa wataalamu wenye ujuzi maalum.

Aidha, alisema mradi wa YEFFA una thamani ya dola za Marekani 1,400,000 (sawa na takribani shilingi bilioni 3.5) na unatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili ukiwa na awamu 11 za udahili. Mradi huo unafadhiliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA), ambalo linaunga mkono juhudi za serikali katika kuendeleza elimu ya ujuzi na sekta ya kilimo.

Kasore alisema mafunzo hayo yanatolewa katika vyuo vinne vya VETA ambavyo ni VETA Kihonda Morogoro, VETA Manyara, VETA Mpanda Katavi na VETA Arusha.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Abra Kingologo, ambaye pia ni mhitimu wa Mzumbe University, alisema baada ya kumaliza shahada yake aliona umuhimu wa kujifunza zaidi kuhusu mitambo ya kilimo.

Alisema kwa sasa amepata ujuzi utakaomwezesha kufanya kilimo cha kisasa katika eneo analotoka.

“Mimi kama msichana sikuona aibu pale serikali ilipotangaza fursa hii. Nikaona ni vyema kujifunza kwa manufaa yangu, taifa na jamii niliyotoka, ingawa baadhi ya wasichana wanaona kama ni ajabu,” alisema

Naye Mkurugenzi Mkazi wa AGRA Tanzania, Vianey Rweyendela, aliwataka vijana waliopata mafunzo kuendelea kuwafundisha wenzao katika maeneo yao ili kuongeza idadi ya vijana wenye ujuzi katika kilimo.

Rweyendela pia aliiomba serikali kuendelea kuwekeza zaidi kwa vijana katika sekta ya kilimo biashara, ujuzi na ubunifu.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI