Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema utafiti unaonesha kuwa kuendesha gari la umeme nchini ni nafuu kwa takribani asilimia 85 kwa kila kilomita ikilinganishwa na gari linalotumia petroli au dizeli.
Mramba ameyasema hayo Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa matumizi ya magari ya umeme nchini kupitia kampuni ya DOW ELEF AUTO EV (ZERA) Limited.
Amesema kwa wastani gari linalotumia mafuta linaweza kugharimu takribani Sh.200 kwa kilomita moja, wakati gari la umeme linatumia karibu Sh.25 pekee kwa kilomita.
“Gharama hii inaonesha wazi kuwa teknolojia ya magari ya umeme ni nafuu zaidi na inaweza kusaidia wananchi kupunguza matumizi katika sekta ya usafiri,” amesema Mramba.
![]() |
| Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba |
Ameeleza kuwa uzinduzi huo ni hatua muhimu katika mageuzi ya sekta ya usafiri nchini na unaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kukuza uwekezaji na kuhamasisha matumizi ya teknolojia safi ya nishati.
Mramba amesema Serikali tayari imeweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya teknolojia hiyo kwa kupitisha Mfumo wa Kitaifa wa Sera ya Magari ya Umeme (National Electric Vehicles Policy Framework) Desemba 2024.
Amesema sera hiyo inalenga kuhamasisha uzalishaji wa magari ya umeme nchini, kuongeza matumizi yake, kuunganisha sekta hiyo na nishati jadidifu pamoja na kujenga miundombinu ya vituo vya kuchaji magari hayo.
Aidha, amesema Tanzania imeendelea kupiga hatua katika uzalishaji wa umeme ambapo uwezo umeongezeka hadi zaidi ya megawati 4,500, huku upatikanaji wa umeme ukifikia asilimia 85.5 mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Mramba, hatua hiyo inalenga kuimarisha sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwamo usafiri wa kisasa wenye gharama nafuu na rafiki kwa mazingira.
Kwa sasa Afrika ina zaidi ya magari ya umeme 30,000, huku Afrika Mashariki ikijitokeza kuwa kitovu cha ubunifu katika sekta hiyo.
Nchini Tanzania, inakadiriwa kuwa tayari kuna zaidi ya magari ya umeme 10,000 yakiwemo pikipiki pamoja na vyombo vingine vya usafiri vya magurudumu mawili na matatu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya DOW ELEF AUTO EV (ZERA) Limited, Emmanuel Kazimoto, amesema kampuni hiyo imeanza na mpango wa kuagiza magari kamili ya umeme, kabla ya kuanza kuleta magari ya kuunganishwa hapa nchini.
Ameongeza kuwa lengo la baadaye ni kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari ya umeme nchini, hatua itakayochochea ajira na kuwajengea vijana wa Kitanzania ujuzi katika teknolojia ya kisasa.



















0 Comments