Header Ads Widget

VIJANA 521 WAONDOKA KWA AJIRA NJE YA NCHI, 45 WAENDA ULAYA


Na OWM-KAM, Dar es Salaam

Serikali imeendelea kufungua na kuimarisha njia salama za uhamiaji wa nguvu kazi kwa kushirikiana na nchi rafiki pamoja na taasisi za kikanda na kimataifa, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha Watanzania wanapata ajira zenye staha, kulindwa haki zao na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia.

Akizungumza katika hafla ya kuwaaga vijana 521 waliopata fursa za ajira nje ya nchi, iliyofanyika Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza ajira kwa vijana.

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha usalama wa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi unalindwa kikamilifu, na kuwahakikishia vijana hao kuwa waende kwa utulivu na kujiamini kwa kuwa Serikali ipo pamoja nao.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ajira, Bi. Jane Sologo, aliwashukuru mawakala binafsi kwa mchango wao mkubwa katika kuwaunganisha Watanzania na ajira za nje.

 Alibainisha kuwa vijana hao 521 wanakwenda kufanya kazi katika nchi za Denmark, Poland, Ujerumani, Bosnia, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mawakala Tanzania, Bw. Abdallah Khaled Mohamed, aliipongeza Serikali kwa ushirikiano wake na mawakala hao, akisema hatua hiyo imeongeza ufanisi na uaminifu katika usimamizi wa ajira za nje.

Miongoni mwa vijana hao walioagwa ni, Raila Shabani, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, anayeelekea Denmark, alisema fursa hiyo itamuwezesha kuongeza ujuzi na maarifa, huku akiwahimiza vijana wengine kutumia ipasavyo fursa zinazotolewa na Serikali.

Katika hatua nyingine Waziri Sangu aliwafahamisha wadau hao kuwa Wizara yake imefanikiwa pia kupata fursa zingine na kwamba ifikapo mwanzoni mwa Aprili 2026, Serikali itangaza ajira 300 kwa Wauguzi wa Kitanzania wanaohitajika kwenda nchini Saudi Arabia kufanya kazi.

Waziri Sangu aliongeza kusema fursa hizi ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuongeza nafasi za ajira kwa watanzania na kusaidia kukuza uchumi wa watanzania.


Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuboresha mazingira wezeshi ili Watanzania wengi zaidi wanufaike na ajira za nje kupitia mifumo salama, halali na yenye staha.

Mwisho.





 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI