Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima media Dodoma
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema bado inakabiliwa na changamoto ya kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kufanya matengenezo ya baadhi ya mitambo mikubwa ya maabara, hali inayochangia kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa vifaa hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkemia Mkuu wa Serikali, Fedelice Mafumiko amesema licha ya wataalamu wa ndani kuendelea kufanya matengenezo ya kawaida na matengenezo kinga ya baadhi ya mitambo na vifaa vya maabara, bado kuna utegemezi wa wataalamu wa nje katika kushughulikia mitambo mikubwa na ya kisasa.
“Ingawa wataalamu wetu wa ndani wamekuwa wakifanya matengenezo ya kawaida na matengenezo kinga ya baadhi ya mitambo, bado tunalazimika kuwaita wataalamu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matengenezo ya mitambo mikubwa, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji,” amesema Dkt. Mafumiko.
Amesema Mamlaka inaendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani ili waweze kufanya matengenezo ya mitambo hiyo hapa nchini.
“Tunaendelea kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi wetu ili wawe mahiri na wabobevu katika kufanya matengenezo na matengenezo kinga ya mitambo, hatua itakayopunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi,” ameongeza.
Aidha, Dkt. Mafumiko amewahimiza vijana wenye ujuzi wa kutengeneza mitambo ya uchunguzi wa maabara kujitokeza kutumia fursa hiyo kwa kutoa huduma za kitaalamu.
MIPANGO YA BAADAYE
Katika hatua nyingine, amesema Mamlaka imepanga kuendelea kuimarisha huduma za maabara kwa kununua mitambo mikubwa ya kisasa pamoja na vifaa saidizi na vitendanishi kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.
Pia Mamlaka inapanga kuimarisha miundombinu kwa kujenga ofisi na maabara katika ofisi za kanda ikiwemo Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini, kwa lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Vilevile, Mamlaka itaendelea kuendeleza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama pamoja na urasimu katika utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau mbalimbali.
Mwisho.
















0 Comments