Mkuu wa Chuo cha FDC Kasulu, Fridegada Mukyamuzi.
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MAFUNZO ya uanagenzi yanayotolewa kwa vijana mbalimbali nchini kupitia vyuo vya maendeleo ya jamii (FDC) yanaelezwa kuchochea utoaji wa idadi kubwa ya vijana wenye taaluma za ufundi ambao wanakubalika na kuingia kwenye soko la ajira nchini.
Wakuu wa vyuo vya maendeleo ya jamii (FDC) mkoani Kigoma wamesema hayo wakati waandishi wa habari walipofanya ziara kutembelea kuona maendeleo na mchango wa vyuo hivyo katika kutoa wataalam wa fani mbalimbali nchini.
Mkuu wa Chuo cha FDC Kasulu, Fridegada Mukyamuzi alithibitisha kuwa chuo chake kimetoa idadi kubwa ya wanafunzi ambao wameombwa kwenye kazi mbalimbali ndani na nje ya mkoa na kwa sasa vijana wengi wamepata mikataba ya kudumu.
Alisema kuwa kuanzia mwaka 2022 hadi sasa Zaidi ya vijana 2300 wamepitia chuoni hapo na kupata kozi mbalimbali za muda mrefu na muda mrefu na wengi wao wamepata ajira au kujiajiri.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya jamii Kihinga wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma, Henry Lyoba alisema kuwa wapo vijana waliosomea ufundi bomba ambao wamepata ajira mbalimbali kwenye mamlaka za maji, wapo vijana wa fani ya umeme ambao wamepata ajira za muda TANESCO, wapo vijana wa ufundi magari na umeme wa magari ambao wamepata ajira kwenye taasisi mbalimbali na kwa sasa wanaendesha maisha yao vizuri kuliko ilivyokuwa awali.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya jamii Kihinga wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma Henry Lyoba.
Mmoja wa wanafunzi waliofaidika na mpango huo ni Luhuda Sabato aliyetumia muda wa miezi sita kujifunza fani ya upishi katika chuo cha FDC Kasulu mkoani Kigoma ambapo baada ya mafunzo yake amebaki chuoni hapo kwa ajira ya muda kwani chuo kimeanzisha mradi wa kutengeneza keki na bidhaa mbalimbali kama biashara ambapo yeye ndiyo mtendaji Mkuu anayeshughulika na jambo hilo akiwasimamia wanafunzi wanaosoma fani ya upishi chuoni hapo.
Mwisho.
Mmoja wa wanafunzi waliofaidika na mpango huo Luhuda Sabato.
Sehemu ya wanafunzi wa chuo cha maendeleo (FDC KASULU) wakiwa kwenye mafunzo kwa vitendo.










0 Comments