Header Ads Widget

MIRADI YA NISHATI YAFUNGUA FURSA ZA AJIRA KWA VIJANA.

 



Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma


SERIKALI imesema kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini unaendelea kufungua fursa nyingi za ajira, mafunzo na ushiriki wa vijana katika kukuza uchumi wa taifa.



Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mussa Makame amesema miradi hiyo si tu inachochea ukuaji wa uchumi wa Taifa, bali pia inalenga kuwajengea vijana uwezo na ujuzi katika sekta ya nishati.


“Ni muhimu kufahamu kuwa takribani asilimia 79 ya nguvu kazi ya TPDC ni vijana. Hii inaonesha dhamira ya Serikali ya kuwaamini na kuwapa nafasi vijana wa Kitanzania kushiriki kikamilifu katika kuendesha sekta ya nishati,” amesema.



Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya TPDC umefungua fursa mbalimbali kwa vijana ikiwemo ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja pamoja na mafunzo ya vitendo kwa vijana wanaoshiriki katika ujenzi wa miradi hiyo.


“Vijana pia wananufaika kupitia zabuni za utoaji huduma katika nyanja mbalimbali kama uhandisi, usafirishaji, ujenzi, ugavi, teknolojia na huduma za kitaalamu,” ameongeza.


Aidha, shirika hilo linaendesha programu ya mafunzo kwa vitendo (Internship Program) ambapo takribani vijana 60 hupata nafasi kila mwaka ya kujifunza na kupata uzoefu katika usimamizi na uendeshaji wa sekta ya nishati, hususan sekta ndogo ya gesi asilia.


Vilevile, miradi hiyo imechangia kuimarisha sekta nyingine za kiuchumi kama viwanda, usafirishaji na hoteli, hali inayowezesha vijana kujiajiri au kupata ajira katika maeneo mbalimbali.


Kwa upande wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), amesema maandalizi yanaendelea ya kuwajengea uwezo vijana watakaoendesha mradi huo mara tu utakapoanza uzalishaji.



“Kupitia programu maalum ya maandalizi ya wataalamu wa mradi wa EACOP, vijana 138 tayari wamepata mafunzo ya vitendo katika taasisi mbalimbali ikiwemo VETA, Arusha Technical College na Uganda Petroleum Institute Kigumba,” amesema.


Ameongeza kuwa vijana hao pia wamepata uzoefu katika miradi ya viwanda vya kuchakata gesi asilia ya Madimba na Songo Songo pamoja na mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam, ikiwa ni maandalizi ya kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi wa EACOP.


Mwisho. 








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI