Header Ads Widget

TFS, LAND AFRICAN SAFARI KUSHIRIKIANA KUKUZA UTALII KUPITIA MBIO ZA CAPE TO CAIRO ARUSHA


Na Mwandishi Wetu, Arusha


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeingia katika mpango wa ushirikiano na kampuni ya Land Africa Safaris ili kukuza utalii wa ikolojia kupitia tukio la Cape to Cairo Arusha International Marathon linalotarajiwa kufanyika Mei 28 hadi 30, 2026 mkoani Arusha.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kilichofanyika Machi 17, 2026 katika Ofisi ya Mhifadhi Mkuu wa Ziwa Duluti, Arumeru.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mhifadhi Mkuu wa Ziwa Duluti, Peter A. Myonga, alisema ushirikiano huo ni fursa muhimu kwa TFS kutumia michezo kutangaza vivutio vya misitu na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea maeneo hayo.



Alisema tukio hilo linatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 5,000 kutoka ndani na nje ya nchi, hatua itakayochochea ongezeko la wageni, muda wa kukaa kwa watalii jijini Arusha na mapato yatokanayo na utalii.

Kwa mujibu wa Myonga, TFS imejipanga kushiriki kikamilifu kwa kutoa ufadhili wa huduma na kifedha, pamoja na kutumia majukwaa mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutangaza utalii wa misitu na nyuki (api-tourism).

Aidha, alisema washiriki wa mbio hizo watapata fursa ya kutembelea vivutio vya misitu ikiwemo Shamba la Miti Meru na Ziwa Duluti kabla na baada ya tukio, huku mipango ikiwekwa kuhakikisha katika msimu ujao wa 2027 njia ya mbio inapita ndani ya hifadhi hizo ili kuongeza mvuto wa utalii.

Aliongeza kuwa TFS itanufaika pia kwa kuanzisha mabanda ya maonyesho, kutengeneza vifurushi vya utalii, huduma za kambi katika eneo la Napuru na kushiriki katika hafla ya Gala Dinner itakayotoa jukwaa la kuitangaza sekta ya misitu na nyuki.

Kwa upande wake, Haffy Mohamed  kutoka Land Africa Safaris alisema wataendelea kushirikiana na TFS kuhakikisha tukio hilo linakuwa chachu ya kukuza utalii wa michezo nchini.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuunganisha sekta ya michezo na utalii ili kuongeza mchango wa rasilimali za asili katika uchumi wa Taifa.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI