Na. Jacob Kasiri - Tarangire.
Ujumbe maalumu Kutoka Serikali ya Zambia ulioongozwa na
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Mhe. Siazongo Siakalenge ambaye pia anashughulikia masuala ya Fedha na Maendeleo ya Uchumi - Zambia umefurahishwa na kustaajabishwa na wingi wa makundi makubwa ya tembo waliyoyaona wakati walipofanya utalii ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire leo machi 18, 2026 wakitokea Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa lengo la kujifunza mikakati na mbinu mbalimbali zinazohusiana na masuala ya Uhifadhi na Utalii nchini Tanzania.
Wakiwa katika Hifadhi ya Tarangire, Mhe. Siakalenge alisema; “Nimefurahishwa na kushangazwa na makundi makubwa ya tembo, hivyo natamani kujua ni mikakati na mbinu gani ambazo mnatumia kuwa na tembo wengi kiasi hicho kwani kila sehemu tuliyopita tumekutana na makundi mengi na tembo wenu wana miili mikubwa.”
“Aidha, pia tumeona “park fees” zenu ziko chini hasa kwa wazawa ili kuhamasisha wazawa wengi kutembelea Hifadhi za Taifa, *kwani tunajua utalii mzuri huanzia nyumbani.* Hivyo hili la bei ya viingilio kuwa ndogo tunalibeba na kwenda kulifanyia kazi katika hifadhi zetu” aliongeza Mhe. Siakalenge.
Akitoa wasilisho kwa niamba ya Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire, Afisa Uhifadhi Mkuu Upendo Massawe alisema ulinzi imara unaotekelezwa na makamanda hao umekuwa ni chapuo la ongezeko la wanyamapori wengi, kuimarika kwa ikolojia na uimarishwaji wa miundombinu pia umepelekea maeneo yetu ya doria kufikika kwa wakati wote kwa mwaka mzima pawe na mvua au kiangazi.
Aidha, Kamanda Massawe aliongeza kuwa, kwa kuwa tembo husafiri umbali mrefu kusaka malisho na maji, ulinzi imara dhidi ya ujangili na udhibiti wa migogoro na binadamu ni muhimu, hivyo tangu 2016 hakuna tukio la ujangili wa tembo ulioripotiwa katika hifadhi hiyo.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Daniel Nuhu Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Hifadhi - TANAPA akihitimisha ziara ya ugeni huo kutoka nchini Zambia kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, alidadavua kuwa ujio huo ni muhimu kwani unaendeleza ushirikiano wa zaidi ya miaka 60 ulianzishwa na waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Julius Kambarage Nyerere na Kenneth Kaunda katika harakati za kupigania Uhuru, sanjari na ushirikiano wa kiuchumi hasa Reli (TAZARA) na bomba la mafuta (TAZAMA).
Ziara hiyo ya Siku tatu ndani ya Hifadhi za Taifa Serengeti na Tarangire iliyoanza machi 16, 2026 ya Ujumbe huo maalumu kutoka nchini Zambia imetamatika leo katika Hifadhi ya Taifa Tarangire.

















0 Comments