Akubali kituo cha taarifa, afungua milango kwa uwekezaji
Matukio Daima, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Heri James, ametangaza mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii ya mkoa huo huku akiahidi kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kukubali kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha taarifa za maendeleo kwa ukanda wa Kusini.
Akifungua mkutano wa wadau wa habari wa Taasisi ya Vyombo vya habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania, MISA-TAN, wakiwemo wahariri, waandishi wa habari na wadau wa habari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, James amesema Serikali ya mkoa huo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.
Amesema tayari Serikali imeridhia ombi la MISA Tanzania la kuanzisha kituo hicho mkoani Iringa na kuitaka taasisi hiyo kuwasilisha maombi rasmi ili mchakato wa kupatiwa eneo uweze kukamilika haraka.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wananchi, hususan katika sekta za kilimo, Teknolojia,afya, elimu na biashara, ambazo ni mhimili wa uchumi wa ukanda wa Kusini.
Katika hotuba yake, James ametumia fursa hiyo kuitangaza Iringa kama kitovu kipya cha uwekezaji nchini, akieleza kuwa uchumi wa mkoa huo umeongezeka kwa kasi kutoka Sh trilioni 4.5 mwaka 2020 hadi kufikia zaidi ya Sh trilioni 6.3 mwaka 2024.
Amesema ukuaji huo umetokana na jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, misitu, mifugo, viwanda pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya barabara, maji na umeme.
“Tunayo fursa nyingi za uwekezaji, kuanzia kilimo cha umwagiliaji, viwanda vya kusindika mazao, utalii hadi sekta ya misitu. Mkoa wetu uko tayari kupokea wawekezaji,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Ameongeza kuwa sekta ya kilimo inaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa huo kwa kuchangia zaidi ya asilimia 85 ya pato la mkoa na kuajiri zaidi ya asilimia 82 ya wananchi.
Aidha, alisema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika huduma za jamii ambapo mabilioni ya shilingi yametumika kuboresha sekta za afya, elimu na maji, hatua inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, upatikanaji wa maji safi umefikia zaidi ya asilimia 80, huku vijiji vyote mkoani humo vikiwa vimeunganishwa na huduma ya umeme, jambo linalorahisisha uwekezaji na shughuli za uzalishaji.
Mapema, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema kituo cha taarifa kinachotarajiwa kujengwa kitakuwa jukwaa la kusambaza taarifa muhimu kwa wananchi zikiwemo bei za mazao, hali ya hewa, teknolojia za kilimo pamoja na masuala ya afya na elimu.
Amesema pamoja na hilo, taasisi hiyo inaendelea kuhamasisha uandishi wa habari wenye mwelekeo wa suluhisho ili kusaidia jamii kupata majibu ya changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amwwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kubadili mitazamo ya wananchi, akisisitiza kuwa maendeleo ya nchi yanahitaji mabadiliko ya fikra hasa kwa vijana.
Mkutano huo umeelezwa kuwa ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na wadau wa maendeleo, huku ukitarajiwa kuchochea uandishi wa habari unaolenga kujenga jamii na kuhamasisha maendeleo endelevu.
Mwisho.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)




0 Comments