Dar es Salaam. Serikali imesisitiza kuwa uamuzi wake wa kumiliki hisa chache katika baadhi ya kampuni nchini na nje ya nchi unalenga kushiriki katika maamuzi ya kimkakati na kuhakikisha uwekezaji wake, ambao kwa sasa umefikia Sh1.94 trilioni, unaleta tija kwa Taifa.
Kauli hiyo ilitolewa Jumanne, Machi 3, 2026 na Bi. Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mashirika ya Kibiashara kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), kuelekea Mkutano wa Wakurugenzi wa Bodi za Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache utakaofanyika Machi 16 hadi 18, mwaka huu.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC 1, Bi. Mauki alikuwa akijibu swali la mtangazaji aliyetaka kufahamu kwa nini serikali inaendelea kubaki na hisa chache badala ya kujiondoa kabisa kwenye baadhi ya kampuni.
“Lengo la Serikali si kuendesha biashara moja kwa moja, bali kulinda maslahi ya Taifa. Kuna kampuni ambazo ni muhimu Serikali kuwa na umiliki wa hisa, hata kama ni asilimia mbili tu,” alifafanua Bi. Mauki.
Kwa mujibu wake, OMH inasimamia jumla ya taasisi 308, ambazo jumla ya uwekezaji wake ni Sh92.3 trilioni.
Kati ya hizo, 252 ni kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa nyingi, huku 56 zikibaki kuwa kampuni ambazo serikali ina hisa chache, yaani chini ya asilimia 51.
Umiliki huu unaiwezesha Serikali kupata gawio na mapato ya kodi, kushiriki katika maamuzi ya bodi, na kulinda rasilimali za kimkakati, hususan katika sekta muhimu kama vile madini na nishati.








0 Comments