Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Janabi, akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amezindua jengo maalum la kisasa la kuhudumia watoto wachanga hususan wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza Februari 28, 2026, hatua inayolenga kuinua huduma za afya ya mama na mtoto katika mkoa huo.
Jengo hilo limejengwa kwa ufadhili wa Doris Mollel Foundation (DMF) kwa kushirikiana na Keep a Child Alive (KCA), likiwa na lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa watoto njiti, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya afya.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Prof. Janabi amesema uwekezaji huo unaonyesha dhamira ya dhati ya wadau wa maendeleo katika kuhakikisha watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wanapata huduma bora, salama na zenye viwango vya kimataifa. Amesisitiza kuwa kuimarisha huduma za watoto wachanga ni msingi wa kujenga kizazi chenye afya na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel, amesema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2015 imepitia mageuzi makubwa kwa lengo la kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati nchini. Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano wa kimkakati na serikali pamoja na wafadhili wa kimataifa, taasisi hiyo imefanikiwa kushawishi mabadiliko ya kisheria kuhusu likizo ya wazazi na kuwezesha upatikanaji wa ufadhili wa kitaifa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya matibabu ya watoto wachanga.
Bi. Mollel amebainisha kuwa ujenzi wa kitengo maalum cha uangalizi wa watoto wachanga (Neonatal Care Unit) ni hatua muhimu katika safari hiyo, akisisitiza kuwa jengo hilo limebuniwa kwa kuzingatia maoni ya moja kwa moja kutoka kwa akina mama wa eneo husika ili kuhakikisha linakidhi mahitaji yao ya kimatendo na hata kiroho. Ameongeza kuwa mradi huo umetokana na ushirikiano wa serikali, wadau wa maendeleo na jamii.














0 Comments