Header Ads Widget

KAMPUNI YA FAIR POINT IRINGA YAADHIMISHA MIAKA 10 KWA MAFANIKIO

  

TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII

NA MATUKIO DAIMA MEDIA 

KAMPUNI ya Fair Point imeadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya matendo ya huruma kwa jamii ya Iringa, ikiwemo kutembelea kituo cha watoto yatima na kutoa misaada, pamoja na kuwapatia viwanja wafanyakazi wake watatu waanzilishi kama sehemu ya motisha kwa mchango wao katika kukuza kampuni hiyo. 

Maadhimisho hayo yaliambatana na uzinduzi wa ofisi kuu mpya ya kampuni hiyo iliyopo jirani na ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa.

 Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Fair Point, Frank Mdesa, alisema kuwa uongozi wa kampuni umeona ni vyema kusherehekea mafanikio ya miaka 10 kwa kurejesha fadhila kwa jamii inayowazunguka.


 Alisema Fair Point ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na wafanyakazi wawili pekee, lakini kwa sasa imekua na kufikia zaidi ya wafanyakazi 40, hatua inayoonesha namna ambavyo kampuni hiyo imeendelea kupanuka na kuimarika katika sekta ya huduma za kifedha nchini.


 “Tumetoka mbali. Tulianza tukiwa wawili tu, lakini leo tunajivunia kuwa na timu ya zaidi ya wafanyakazi 40. Haya ni mafanikio makubwa kwetu, na tunamshukuru Mungu pamoja na wateja wetu kwa kutuamini,” alisema Mdesa.


 Aliongeza kuwa kampuni hiyo inayojishughulisha na utoaji wa huduma za kifedha imefanikiwa kupanua wigo wa huduma zake katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara ikiwemo Iringa, Dodoma, Morogoro na Tanga, huku mpango wa baadaye ukiwa ni kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi katika mikoa yote nchini. 


Kwa mujibu wa Mdesa, maadhimisho ya miaka 10 hayakulenga kusherehekea tu mafanikio ya kibiashara, bali pia kuimarisha mshikamano miongoni mwa wafanyakazi na kuwajengea uwezo kupitia mafunzo mbalimbali.


 Alisema katika kipindi hicho cha maadhimisho, wafanyakazi walipatiwa elimu kuhusu sheria za kazi, masuala ya hifadhi ya jamii kupitia NSSF, pamoja na mada nyingine muhimu zinazohusu ustawi wao kazini.


 “Tunaamini kuwa mafanikio ya kampuni yanatokana na nguvu ya pamoja ya wafanyakazi ndiyo maana tumeona ni muhimu kuwapatia elimu itakayowawezesha kufahamu haki na wajibu wao, sambamba na kuwajengea uelewa wa masuala ya hifadhi ya jamii,” alisisitiza. 


Mbali na kutoa mafunzo, kampuni hiyo pia ilitembelea kituo cha watoto yatima kilichopo mkoani Iringa na kutoa misaada mbalimbali ikiwemo mahitaji ya chakula, mavazi na vifaa vingine muhimu kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao.

 Mdesa alisema kitendo hicho ni sehemu ya dhamira ya kampuni kushiriki katika shughuli za kijamii na kusaidia makundi yenye uhitaji maalum.


 Aidha, katika kuonesha kuthamini mchango wa wafanyakazi waliokuwa waanzilishi wa kampuni hiyo, uongozi wa Fair Point uliwapatia viwanja watatu kati ya wafanyakazi wa mwanzo kama motisha na shukrani kwa uaminifu na juhudi zao.

Mdesa alisema utoaji wa viwanja hivyo ni ishara ya kutambua mchango wao mkubwa katika safari ya ukuaji wa kampuni tangu ilipoanzishwa hadi kufikia hatua ya sasa.


Maadhimisho ya miaka 10 ya Fair Point yameacha alama si tu kwa wafanyakazi wake bali pia kwa jamii ya Iringa, yakionesha kuwa ukuaji wa biashara unaweza kwenda sambamba na uwajibikaji kwa jamii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI