Na Lilian Kasenene, Morogoro
WATU wawili wamefariki Dunia mkoani Morogoro katika matukio mawili tofauti likiwemo la mtoto wa miaka 12 kujinyonga baada ya kukemewa na wazazi wake ili kuacha vitendo vya udokozi.
Kamanda wa polisi mkoani hapa Alex Mkama alisema tukio hilo la kujinyonga limebainika mapema Asubuhi Machi, 23, 2026 huko katika kitongoji cha Kaloleni, kata ya Italagwe, Wilaya ya Gairo.
Kamanda huyo alimtaja mtoto huyo Rajabu Ally Mohammed (12), mkazi wa Ijava ambaye amekutwa akiwa amekufa kwa kujinyonga nyuma ya nyumba yao wanayoishi.
Mkama alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo siku ya machi, 22, 2026 alikemewa na wazazi wake kuacha vitendo vya udokozi baada ya kukamatwa na wenzake wawili wakiwa wameiba mahindi mabichi.
Alisema kitendo cha kukemewa kilimjaza hasira na kuamua kujiua kwa kutumia mkanda wa suruali yake.
Katika tukio la pili kamanda huyo alisema jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawatafuta ndugu wa mtu mmoja amekufa kwa ghafla akiwa katika stand ya mabasi ya Msamvu, Manispaa ya Morogoro.
Alisema tukio hilo limetokea Machi, 22,2026 jioni katika eneo la stand kuu ya mabasi yaendaayo Mikoani, eneo la Msamvu Kata ya Mafisa, Manispaa Morogoro.
Alisema Marehemu amefahamika kwa majina kwenye vitambulisho vyake kuwa ni Reuben Masimba Chedego (70), mkulima na mkazi wa Chalinze.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu amekufa ghafla muda mfupi baada ya kushuka kwenye gari ya abiria akitokea Dar es Salaam kwenda Morogoro.
Alisema marehemu huyo alipokwenda kupata haja ndogo aliishiwa nguvu, akadondoka na kisha kupelekwa hospital ya mkoa kwa haduma. Hata hivyo, imethibitika kuwa alikuwa tayari alikufa kabla ya kufikishwa hospitalini hapo.
Alisema Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi zaidi na utambuzi kutoka kwa ndugu zake.
Mwisho.






0 Comments