Header Ads Widget

WANAHABARI SINGIDA WAJENGEWA UWEZO MAFUNZO MITANDAO YA KIJAMII

 

Na Elisante John, Singida

‎‎Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwa kufungua na kutumia kikamilifu akaunti za mitandao ya kijamii, hatua itakayowarahisishia upatikanaji na usambazaji wa taarifa sahihi kwa umma na kwa wakati.

‎Wito huo umetolewa leo Machi 23, 2026 na Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Media Brain, Jesse Kwayu, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wanahabari wa mkoa wa Singida.

‎Mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa Regency Hotel yamewakutanisha jumla ya wanahabari 21, yakilenga kuwajengea uwezo katika uandishi na uripoti wa habari za kidijitali.

‎Akizungumza katika mafunzo hayo, Kwayu amesema kasi ya usambazaji wa taarifa kupitia mitandao ya kijamii inaongezeka duniani kote, hivyo ni muhimu kwa wanahabari kujiimarisha katika matumizi ya majukwaa hayo ili kufikia hadhira pana zaidi.

Amefafanua kuwa matumizi sahihi ya mitandao hiyo yatasaidia kupunguza upotoshaji wa taarifa na kuongeza uaminifu wa vyombo vya habari mbele ya jamii.

‎Kwa upande wake, Mkuu wa Itifaki wa shirika hilo, Neville Meena, amewahimiza wanahabari wa Singida kuibua na kuripoti habari zenye maslahi kwa jamii kupitia majukwaa ya kidijitali.

‎Meena amesema hatua hiyo itasaidia kuutangaza mkoa wa Singida pamoja na shughuli za maendeleo zinazofanywa na viongozi wake, hivyo kuvutia uwekezaji na fursa mbalimbali.

Naye Meneja Miradi wa Konrad Adenauer Stiftung, Damas Nderumaki, amesema taasisi hiyo imefadhili mafunzo hayo ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha sekta ya habari nchini.

‎Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwake nchini mwaka 1960, shirika hilo limekuwa likishirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na vyuo vya elimu katika kukuza demokrasia na maendeleo ya jamii.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI