Header Ads Widget

MISITU KUIOKOA

Makamu Rais wetu, maagizo ametoa,

Kutunza mazingira tu, misitu kuiokoa,

Tusiwe hivihivi tu, kufanya ya kupotoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Ni Misitu duniani, siko agio metoa,

Akiwa Lindi mjini, maelekezo katoa,

Mijini na vijijini, ni vema tukajitoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Maeneo mengi wazi, miti tulishaitoa,

Sasa kwetu sote kazi, mazingira kuokoa,

Kutunza hiki kizazi, wakati tukijitoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Upotevu wa misitu, uasili unatoa,

Mvua maeneo yetu, uoto yanaondoa,

Shida inakuja kwetu, na rutuba kupopoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Mhe Nchimbi kasisitiza, takwimu akizitoa,

Miti tunayopoteza, hekta nyingi twaondoa,

Tusije kujituliza, twapaswa kujiokoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Laki nne na sitini, hekta tunaondoa,

Hii ni kote nchini, hakuna palipopoa,

Hivyo jambo la thamani, miche mingi kuitoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Miche upatikanaji, uhakika ametoa,

Huo ni uwekezaji, serikali kujitoa,

Ili miti wapandaji, ardhi yetu kuokoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Vitalu viongezeke, miti mingi kuitoa,

Wala muda isifike, watu wanaojitoa,

Kupanda miti wachoke, miche kushindwa kutoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Pia nishati salama, sote tuweze jitoa,

Kuitumia ni njema, misitu inaokoa,

Hapo ndipo tutakoma, uoto kuuondoa

Kupika siyo mkaa, kuna majiko watoa,

Ya gesi sana yafaa, na moshi bila kutoa,

Pika bila kuchakaa, moshi machozi kutoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Kuyatunza mazingira, wito jinsi ametoa,

Hilo kwetu jambo bora, tena la kujiokoa,

Kiangazi cha kukera, nacho yatakiondoa,

Misitu kupukutika, liwe jambo la zamani.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

Post a Comment

0 Comments

MAGAZETI

NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI