Na Mwandishi Wetu, Lindi
MAKAMU wa Rais, Mhe Emmanuel Nchimbi, amezindua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa 2026, akionya kuwa kasi ya upotevu wa misitu nchini imefikia hekta 460,400 kwa mwaka na kuwataka Watanzania kuchukua hatua za haraka kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa uchumi na mazingira.
Akizungumza leo Machi 19, 2026 katika Uwanja wa Ilulu, Lindi, Nchimbi alisema misitu si tu chanzo cha maisha bali ni mhimili wa uchumi endelevu, akibainisha kuwa sekta hiyo inachangia asilimia 3.5 ya pato la taifa, na kufikia hadi asilimia 20 inapojumuishwa thamani ya huduma za mifumo ikolojia zisizo na bei ya soko.
“Leo tunazindua kampeni ya upandaji miti kitaifa ili kuongeza uhamasishaji wa wananchi kupanda na kutunza miti. Hatuwezi kuendelea kuvumilia upotevu huu wa misitu,” alisema.
Alifafanua kuwa Tanzania ina takribani hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo lote la nchi kavu, lakini sehemu kubwa inakabiliwa na vitisho vya shughuli za binadamu zikiwemo uvamizi, uchomaji moto, ufugaji holela na matumizi makubwa ya kuni na mkaa.
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais alisisitiza kuwa kampeni hiyo ni utekelezaji wa moja kwa moja wa maono ya Samia Suluhu Hassan kupitia ajenda ya “Tanzania ya Kijani”, akitaja kuwa zaidi ya miti milioni 113 tayari imepandwa tangu mwaka 2023.
Alitoa maagizo kwa viongozi wa mikoa na halmashauri nchini kuhakikisha wanatekeleza mikakati madhubuti ya upandaji miti kwa kuzingatia ekolojia ya maeneo husika, huku akisisitiza elimu kwa jamii na usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji.
Makamu wa Rais pia aliielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kuimarisha tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto za wakulima wa miti na kubaini aina sahihi za miti kwa kila eneo.
Aidha, aliagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuongeza uzalishaji wa miche ya miti na kuimarisha vitalu nchini ili kuhakikisha upatikanaji wa miche bora kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe Nchimbi alitumia jukwaa hilo kuelekeza Wizara ya Nishati kuharakisha utekelezaji wa mradi wa umeme wa gridi ya taifa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, akisisitiza kuwa ni agizo la kipaumbele la Serikali.
“Waziri wa Nishati hana hiari, ni lazima asimamie jambo hili kwa haraka kama alivyoelekeza Rais,” alisisitiza.
Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Dkt. Ashatu Kijaji, alisema mkoa wa Lindi umebarikiwa kuwa na rasilimali kubwa za misitu, ukiwemo ukanda mpana wa mikoko na misitu ya miombo, na kwamba maadhimisho hayo yameutoa fursa ya kujifunza na kuhamasisha uhifadhi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, alisema zaidi ya hekta milioni 1.058 za misitu zimehifadhiwa kisheria mkoani humo, huku akibainisha kuwa misitu ya vijiji imekuwa chachu ya maendeleo kupitia mapato ya zaidi ya Sh bilioni 3.2 kwa mwaka.
Aliongeza kuwa mkoa huo tayari umepanda miti milioni 5.7 kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2024/25, sawa na asilimia 64 ya lengo, huku asilimia 88 ya miti hiyo ikionesha kuota vizuri.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe Timotheo Mzava (Mb), alisema Bunge litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha sera na mikakati ya uhifadhi wa misitu inatekelezwa ipasavyo.
“Tutahakikisha Serikali inatimiza wajibu wake wa kisera, kisheria na kibajeti katika sekta ya misitu,” alisema.
Maadhimisho ya mwaka huu yenye kaulimbiu ya "Misitu ni Uchumi Endelevu, Tuihifadhi kwa Maendeleo ya Taifa" yatafikia kilele Machi 21, yakitarajiwa kuambatana na kampeni ya kitaifa ya upandaji miti inayolenga kuongeza uoto wa asili na kulinda mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.



















0 Comments