Header Ads Widget

𝐖𝐀𝐍𝐀𝐖𝐀𝐊𝐄 𝐓𝐅𝐒 𝐖𝐀𝐆𝐔𝐒𝐀 𝐌𝐈𝐎𝐘𝐎 𝐘𝐀 𝐖𝐀𝐆𝐎𝐍𝐉𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐃𝐀𝐁𝐀

 


-𝙒𝙖𝙩𝙤𝙖 𝙢𝙞𝙨𝙖𝙖𝙙𝙖 𝙫𝙞𝙩𝙪𝙤 𝙫𝙮𝙖 𝙖𝙛𝙮𝙖 𝙠𝙪𝙚𝙡𝙚𝙠𝙚𝙖 𝙎𝙞𝙠𝙪 𝙮𝙖 𝙒𝙖𝙣𝙖𝙬𝙖𝙠𝙚 𝘿𝙪𝙣𝙞𝙖𝙣𝙞


Na Mwandishi Wetu


MADABA, RUVUMA. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kupitia Shamba la Miti Wino kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, wametoa msaada wa mahitaji muhimu kwa wagonjwa na watu wasiojiweza katika vituo vya afya vya Mtyangimbole na Madaba, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Msaada huo umetolewa na watumishi wanawake wa TFS katika zoezi lililolenga kugusa maisha ya watu wenye uhitaji huku likionesha mshikamano wa kijamii kwa vitendo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Wino mapema Wiki hii, Mhifadhi Martha Ndyetabula alisema hatua hiyo inalenga kuwafikia wagonjwa na watu wasiojiweza ili nao wajione kuwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo muhimu kimataifa.




Alisema wanawake wana nafasi kubwa katika kuleta faraja na matumaini kwa jamii, hivyo ni muhimu kutumia maadhimisho hayo kuonesha upendo, huruma na mshikamano kwa vitendo.

“Kama wanawake tunapaswa kutumia nafasi hii kuonesha upendo na mshikamano kwa wengine. Maadhimisho haya yana maana zaidi pale yanapogeuzwa kuwa matendo halisi yanayogusa maisha ya watu wenye uhitaji,” alisema Ndyetabula.

Aliongeza kuwa TFS itaendelea kushirikiana na jamii katika shughuli mbalimbali za kijamii zinazolenga kuboresha ustawi wa wananchi na kuimarisha mahusiano kati ya taasisi na jamii inayozunguka maeneo ya shughuli zake.

Kwa upande wao, baadhi ya wagonjwa na wananchi waliopokea msaada huo walishukuru TFS na Halmashauri ya Madaba kwa kuwajali watu wenye uhitaji, wakisema msaada huo umewapa faraja na kuongeza matumaini wakati wa matibabu.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi, ikiwa ni jukwaa la kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii na kusisitiza usawa wa kijinsia.

Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi wa Kufikia Dira ya 2050.”








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI