Header Ads Widget

DR. KIJAJI: TANZANIA YAENDELEA KUNG'ARA KIMATAIFA NA KUWA KITUO BORA CHA UTALII NA UHIFADHI DUNIANI



Na. Calvin Katera - Arusha. 


Waziri wa Maliasili na utalii nchini Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema kuwa Tanzania imeendelea kuwa kituo bora cha utalii Duniani kutokana na wingi wa Tuzo inazoendelea kuzipokea kupitia taasisi na majukwaa ya kimataifa. Hali hii imechagizwa na ulinzi imara unaofanya na maafisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi na Misitu nchini.

Kauli hiyo aliitoa leo machi 03, 2026 katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani iliyofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane vilivyopo Njiro jijini Arusha.

Katika  hafla hiyo Dkt. Kijaji alisema, "Tanzania imeendelea kung'ara kimataifa kwa kuwa kituo bora cha utalii duniani. Hali hii  inathibitishwa na uwepo wa tuzo tunazoendelea kuzipata kupitia taasisi na majukwaa mbalimbali duniani. Hivi karibuni tumeshinda tuzo tano muhimu za utalii duniani, hakika sote tunapaswa kuendelea kutambua mchango mkubwa wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kunadi vivutio hivyo.”





Sambamba na hilo Dkt. Kijaji aliongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na usimamizi madhubuti wa maeneo ya hifadhi, mapambano dhidi ya ujangili pamoja na ushirikishwaji wa jamii katika kulinda na kuhifadhi maliasili.

“Wizara kupitia taasisi zake za TANAPA, TAWA, TFS na NCAA zitaendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na matumizi sahihi ya teknolojia ili kuhakikisha maliasili hizo zinaendelea kuwa na mchango katika uchumi wa Taifa letu”, aliongeza Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini, Dkt. Alexander Lobora alisema kuwa kuimarika kwa hali ya wanyamapori nchini ni matokeo ya ushirikiano kati ya serikali, wadau wa uhifadhi na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi. 

Aidha, Dkt. Lobora alisema, “Ikolojia ya mimea imeimarika, halikadhalika idadi ya wanyamapori imeongezeka kutokana na matumizi ya TEHAMA, jambo linaloendelea kuipa Tanzania heshima katika medani za kimataifa.”






Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Nkoba Mabula, alisema kuwa wizara itaendelea kusimamia sera na mikakati itakayohakikisha uhifadhi unaenda sambamba na maendeleo ya wananchi. 

Hata hivyo Bw. Mabula, aliendelea kusisitiza kuwa uchumi wa jamii na uhai wa mfumo wa ikolojia haviwezi kutenganishwa na siku hii. Maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani ni jukwaa la kuwasemea wanyamapori hao wasioweza kujisemea wenyewe.

Maadhimisho hayo yaliyobeba kauli mbiu isemayo "Mimea Dawa na Manukato: Kutunza Afya, Kuhifadhi Urithi na Kuboresha na Maisha" pia ilihudhuliwa na Mhe. Joseph Mkude Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, 

Wakurugenzi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Makamishna wa Uhifadhi kutoka TANAPA, NCAA, TAWA, Makamishna Waandamizi, Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi na Misitu, Wakuu wa Vyuo na Taasisi, Viongozi wa Dini na wadau mbalimbali kutoka sekta ya Uhifadhi na Utalii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI