TAREHE 10 Machi 2026, katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, imefanyika hafla fupi ya kumuaga Deo Chami, mmoja wa watu wenye mahitaji maalum, kabla ya kuanza safari yake ya kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Marangu.
Hafla hiyo imefanyika chini ya mapokezi ya uongozi wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, huku lengo la safari hiyo likiwa kuhamasisha utalii wa ndani kwa watu wenye mahitaji maalum na kuonesha kuwa mlima hauna kikwazo kwa mtu yeyote mwenye dhamira ya kufikia lengo lake.
Safari ya Deo imewezeshwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo Tanzania Forest Services (TFS) na Bodi ya Maji Bonde la Pangani, pamoja na wadau wengine wa sekta ya utalii na uhifadhi.
Ushirikiano huo unaonesha mshikamano wa wadau katika kuendeleza na kuunga mkono utalii jumuishi unaowapa nafasi watu wenye mahitaji maalum kushiriki kikamilifu katika shughuli za utalii.
Aidha, Deo anapanda Mlima Kilimanjaro kwa siku sita kupitia lango la Marangu kwa uratibu wa kampuni ya utalii Africa Scenic Safaris.
Ameagwa na kusindikizwa na wenzake kutoka katika makundi yenye mahitaji maalum waliokuja kumtia moyo, huku wengi wao wakihamasika kushiriki katika shughuli kama hizi siku zijazo.
Safari ya Deo inaonesha kuwa utalii ni jukwaa la ushirikishwaji wa watu wote, na kwamba Mlima Kilimanjaro hauna kikwazo kwa mtu yeyote mwenye ndoto na dhamira ya kufika kileleni.












0 Comments